AJIUA BAADA YA KUFUMANIWA NA MKEWE AKITONGOZA NA KUHONGA MWANAFUNZI

 


Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV


MKAZI wa Mtaa wa Kanisa B wilayani Ludewa mkoani Njombe aliyefahamika kwa jina la John Mhagama( 42) amejiua kwa kunywa sumu baada ya kufumaniwa na mkewe akiwa kwenye  mazungumzo ya kimapenzi na binti wa kidato cha kwanza anayeishi jirani na nyumba yao.


Kwa mujibu wa taarifa zinaelezwa kwamba Mhagama alikuwa na kawaida kila inapofika nyakati za jioni alikuwa akiaga anakwenda kununua mkaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kumbe alipokuwa akienda huko anakutana na binti huyo na kumpa fedha.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issa amethibitisha kutokea tukio hilo na kuongeza kuwa siku ya tukio marehemu huyo alienda kununua mkaa kama kawaida yake lakini mkewe alikuwa akimfuatulia kwa nyuma.

Ameongeza baada ya kufuatilia alimuona mumewe huyo 'akipiga stori' na binti na kumpa fedha Sh.5,000 huku akimbembeleza kumkubalia ombi lake la kuwa na mahusiano ya kimapenzi kwani amekuwa akichukua fedha zake pasipo kumtimizia.

Kamanda ISSA ameongeza hata hivyo mkewe huyo alijitokeza na kuanza kumlaumu mumewe kwa kitendo alichofanya lakini kwa hasira mumewe huyo alimpiga mkewe na kisha kurudi zake nyumbani.

Aidha kwa mujibu wa maelezo ya mkewe huyo amedai kuwa kutokana na hasira alizokuwa nazo mumewe yeye hakutaka kurejea nyumbani kwa muda ule lakini baada ya muda kidogo alipigiwa simu na shangazi wa marehemu akimjulisha mumewe ana hali mbaya, hivyo akafika nyumbani na kumpeleka hospitali ambako ndiko mauti ilimkuta.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Issa ameitaka jamii kutokuwa na wivu uliopitiliza kwani mara nyingi matokeo yake huwa mabaya na wakati mwingine husababisha watu kujeruhiana na pengine kusababisha vifo.


Chanzo- Michuzi Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post