BIBI AUAWA KWA KUPIGWA AKITUHUMIWA MSHIRIKINA BUKENE SHINYANGA


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP Janeth Magomi

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, linawasaka watu ambao bado hawajafahamika kwa tuhuma za mauaji ya Bibi Sophia Dotto (66) mkazi wa kijiji cha Kazuni Kata ya Bukene wilayani Shinyanga.

Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 2 usiku nyumbani kwa Bibi huyo ambapo watu wasiojulikana, walifika nyumbani kwake na kisha kutekeleza mauaji hayo ya kinyama kwa kumpiga kichwani na vitu vizito na kusababisha mauaji.

Akielezea tukio hilo Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kazuni Juma Shija, amesema Bibi huyo mwenye umri wa miaka (66) alikuwa akiishi yeye na mchungaji wake wa mifugo nyumbani kwake, na ilipofika majira hayo ya saa 2 usiku ndipo yalipotokea hayo akituhumiwa kuwa ni mshirikina.

 “Baada ya kukuta Bibi huyo akiwa amefariki dunia, nilitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walifika kijiji majira ya saa 8 usiku wakauchukua mwili wa marehemu,”amesema Shija.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kubainisha kuwa upelelezi wa awali inasemekana Bibi huyo ameuawa kwa imani za kishirikina, na kubainisha kuwa Jeshi hilo linawasaka watu wote ambao wamehusika na mauaji hayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post