NYUMBA YATEKETEA KWA MOTO MJINI SHINYANGA ..ZIMAMOTO WALALAMIKIWA "WAPO HAPA HAPA MJINI WAMEFIKA BAADA YA SAA MOJA"Muonekano vitu vya ndani vikiwa vimeteketea na moto.
Muonekano wa nyumba ambayo imeteketeza vitu ndani baada ya kuteketea moto maeneo ya Majengo Mapya Manispaa ya Shinyanga.

Muonekano wa nyumba ambayo imeteketeza vitu ndani baada ya kuwaka moto maeneo ya Majengo Mapya Manispaa ya Shinyanga.

Muonekano vitu vya ndani vikiwa vimeteketea na moto.

Viatu vikiwa vimeteketea na moto

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

WATU wanne ambao ni wakazi wa Majengo mapya Manispaa ya Shinyanga, wamenusurika kifo mara baada ya nyumba yao kuteketea  kwa moto, huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likinyooshewa kidole kuchelewa kufika kwenye matukio.

Tukio la nyumba hiyo kuwaka moto limetokea leo Septemba 8, 2022 majira ya saa 7 mchana.

Shuhuda wa tukio hilo Elias Kamoga, amesema walifika eneo la tukio mapema na kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na uokoaji, lakini ikapita takribani saa nzima hawajaonekana eneo la tukio huku Moto huo ukiendelea kuteketeza vitu ndani.

Amesema endapo Jeshi la Zimamoto na uokaji lingefika eneo la tukio kwa wakati Moto huo usingeweza kuteketeza vitu ndani, bali vingeokolewa na kutoa wito kwa Jeshi hilo libadilike na kufika kwenye matukio kwa wakati.

“Hapa Shinyanga hatuna Jeshi la Zimamoto bali tuna ofisi tu, haiwezekani kila tukio la Moto wanachelewa kufika kwa wakati na wapo hapa hapa mjini, jana tu kuna nyumba imewaka Moto huko Ndala na kusababisha kifo cha mwananchi mmoja yote hii ni kwa sababu ya uzembe wa Jeshi hili la Zimamoto,” amesema Kamoga.

Naye Mama mwenye nyumba hiyo Ester Mbasa, amesema yeye alikuwa dukani kwake na nyumbani aliwaacha watu wanne akiwamo na baba mkwe wake, na alipopewa taarifa na majirani zake kuwa nyumba yao inawaka moto, ndipo akafika na kukuta moto umeshika kasi huku ukiteketeza vitu ndani.

Amesema anamshukuru Mungu kwa sababu hakuna mtu yoyote kwenye familia yake ambaye amedhurika na tukio hilo mbali na vitu vyao vya ndani kuteketea moto, na kutoa wito kwa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Shinyanga wawe wanawahi kwenye matukio ya majanga ya moto.

Kwa upande wake Mrakibu wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoani Shinyanga Ramadhani Kamo, amesema baada ya kufika eneo la tukio walifanikiwa kuuzima moto huo, lakini vitu vingi vya ndani vimeteketea moto, huku chanzo chake bado wanaendelea kukichunguza.

Aidha, amesema Zimamoto mkoani humo wanakabiliwa na upungufu wa magari ya kuzimia moto, ambapo wana gari moja na lenyewe ni bovu, na ndiyo sababu wamekuwa wakichelewa kufikia maeneo ya matukio ya moto, mpaka waazime gari kutoka Jeshi la wananchi (JWTZ) pamoja na kiwanda cha mtu binafsi cha Gaki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post