GGML MDHAMINI MKUU WA MAONESHO YA TANO YA KITAIFA YA TEKNOLOJIA YA MADINI -GEITA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo (kushoto) akimsikiliza Ofisa Mwandamizi masuala ya Uwekezaji kwa jamii kutoka Kampuni ya Geita Gold Mining Ltd. (GGML), Masaki Godlove (kulia) aliyekuwa akitoa maelezo namna kampuni hiyo inavyozingatia masuala ya uwekezaji kwa jamii. Jana Mbibo alitembelea banda la GGML ambao ni wadhamini wakuu wa Maonesho ya kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili Geita.
Mratibu wa Miradi inayofadhiliwa na Geita Gold Mining Limited (GGML) fedha za Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR), Moses Rusasa (kushoto) akifafanua namna kampuni hiyo inavyoshirikiana na serikali ya mkoa wa Geita kufadhili miradi mbalimbali kupitia Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).
Mratibu wa Miradi inayofadhiliwa na Geita Gold Mining Limited (GGML) fedha za Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR), Moses Rusasa  akifafanua namna kampuni hiyo inavyoshirikiana na serikali ya mkoa wa Geita kufadhili miradi mbalimbali kupitia Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).



Na Mwandishi Wetu - Geita

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGM) kwa mwaka wa tano mfululizo imejitosa kuwa mdhamini mkuu wa Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini ambayo mwaka huu yanafanyika katika viwanja vya Ukanda wa Uwekezaji (EPZ) Bombambili mkoani Geita.


Mwaka huu, GGML imekuwa mdhamini mkuu tena katika maonesho hayo yanayotumika kuonesha teknolojia zinazotumika katika sekta ya uchimbaji pamoja na kuwezesha kliniki za biashara kwa wajasiriamali na kampuni zenye uhitaji na fursa zinazopatikana katika mgodi wa GGML.


Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 27 Septemba 2022 na kufikia tamati tarehe 8 Oktoba 2022, yatatoa fursa kubwa kwa washiriki kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa katika uchimbaji wa madini.

Kampuni ya GGML inaungana na kampuni 600 zinazoshiriki maonesho ya mwaka huu ikiwa na mifumo na teknolojia za kisasa kwa ajili ya kuwaonesha wadau hususani wachimbaji wadogo.


Akizungumzia udhamini wa GGML katika maonesho hayo, Makamu Rais wa Kampuni Anglo Gold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa nchi za Ghana na Tanzania, Simon Shayo amesema kampuni hiyo inafarijika kuwa mdhamini mkuu wa maonesho hayo.


Alisema maonesho hayo ya teknolojia ya madini ambayo yalianza kidogo kidogo miaka mitano iliyopita, ni wazo zuri ambalo Serikali ya mkoa wa Geita na wadau wengine walikuja nalo.


“Tunafarijika kwamba tulihusishwa kama mmoja wa wadhamini wakubwa kuanzia mwanzoni lakini pia tunatambua kwamba wadau wengine ambao hawapo hata kwenye sekta ya madini kama mabenki na wadau wengine waliona umuhimu wa kushiriki si tu kudhamini lakini pia kuleta bidhaa zao kwenye maonesho haya na kuzionesha.


“Wito wetu kwa wadau wote hata wale ambao hawapo kwenye sekta ya madini, tunawaalika waungane na serikali ya mkoa wa Geita na sisi kama GGML tutaendelea kuwepo wakati wote kuhakikisha maonesho haya yanakuwa makubwa, yanakuwa na tija na yanakuwa ya kimataifa,” alisema Bw. Shayo.


Aidha, akizungumzia udhamini huo wa GGML, Naibu Katibu Mkuu wa Madini, Msafiri Mbibo amesema GGML wanafanya vizuri sio tu kwa namna wanavyoonesha utayari wa kufadhili bali mwaka hata mwaka kwa ufadhili wao umewezesha maonesho hayo kukua.


“GGML wanatuwezesha ili tujenge uwezo kwa washiriki wengi zaidi wa maonesho ambapo sio GGML peke yake bali na hata watu wengine washiriki kwa manufaa ya nchi nzima na watu wote,” alisema.


Aidha, Meneja wa Kampuni ya Blue Coast Investment Limited ambayo ni mmoja wa wakandarasi wa kampuni ya GGML, Jeremiah Musa, alisema wamefanikiwa kupata zabuni mbili kutoka GGML ambazo ni kusambaza mafuta pamoja na kusafirisha wafanyakazi wa kampuni hiyo.


“Mbali na kusafirisha asilimia 30 ya mafuta ndani ya GGML pia wametupatia mafunzo mbalimbali jambo ambalo limetusaidia kampuni yetu kukua kwa haraka na kupata fursa ya kujitanua na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania kwani mpaka sasa tuna wafanyakazi 400 walioajiriwa,” amesema.


Naye Msimamizi wa shughuli za kihandisi African Underground Mining Services (AUMS), Redempta Samky amesema kampuni hiyo ambayo inahusika na kutoa huduma za uchimbaji na uendeshaji wa migodi hasa chini ya ardhi (underground), imezidi kukua kutokana na GGML kuwaongezea miradi mbalimbali.


“GGML wametusaidia kukua kama kampuni kwa sababu tulianza na mradi mmoja wa Star and Comet ambao walitupatia, tukaendesha vizuri tukapata mradi mwingine wa Nyankanga ambao ndani yake kulikuwa na miradi mitatu zaidi. Sasa hivi tumeanzisha mradi mpya wa Geita hill ... kwa hiyo huu wote ni ukuaji kwamba GGML wanatuamini ndio maana tunaendelea kutoa huduma.


“Mpaka sasa tuna wafanyakazi zaidi ya 200, tulianza mwaka 2016 kufanya kazi hapa GGML, kwa hiyo sisi ni watoa huduma wa GGML,” alisema.


Maonesho hayo ya tano ya kitaifa ya teknolojia ya madini kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya “Madini na fursa za uchumi ajira kwa maendeleo endelevu”.


GGML imekuwa kinara wa uwekezaji kwenye jamii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ambapo vipaumbele vikuu vimekuwa ni miradi ya afya, elimu, maji, barabara, miradi ya kukuza kipato na miradi mingine mingi ya kijamii ili kuhakikisha jamii mwenyeji inapata maisha bora.


Mapema mwaka huu, kampuni ya GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka wa fedha 2020/2021 baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa mapato (kodi) na uendelezaji wazawa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments