**********************
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeshiriki katika maonesho ya wakulima Nanenane katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Akizungumza katika Maonesho hayo jana Agosti 8,2022, Meneja wa Kanda ya Kusini (TBS), Bi.Amina Yassin amesema wametoa elimu ya viwango na udhibiti ubora kwa wananchi kwenye maonesho hayo na wengine wameweza kupewa huduma ya namna wanavyoweza kuzalisha bidhaa ambazo zinakidhi viwango.
Amesema kuwa baadhi ya wajasiriamali waliodhuhuria maonesho hayo wamepatiwa elimu kuhusu utaratibu wa kupata alama ya ubora na walielekezwa kwenda SIDO ili waweze kupatiwa barua ya utambulisho kwaajili ya kupewa alama ya ubora bure kwa miaka mitatu ya mwanzo.
"Ni faida kubwa kwa wajasiriamali kupata alama ya ubora kwenye bidhaa zao kwasababu itasaidia kushindana sokoni na kupata wateja wengi na pia kupata faida ya kutosha kuliko yule ambaye anazalisha bidhaa ambayo haina alama ya ubora ya TBS". Amesema Bi.Amina.