NHC KUMUENZI RAIS SAMIA KUPITIA MRADI WA SHS

Meneja habari na mahusiano wa NHC Muungano Saguya akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dodoma katika ukumbi wa Habari-Maelezo 

Na Dotto Kwilasa, DODOMA 
                                                                                              

MENEJA habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)Muungano Saguya ameeleza utekelezaji wa shughuli na mwelekeo wa shirika hilo kwa mwaka 2022/2023 huku akitaja vipaumbele kuwa ni  kuanza utekelezaji wa Sera ya Ubia itakayoruhusu Sekta Binafsi kushiriki katika uendelezaji wa maeneo ya Shirika.

Amesema leo Agosti 9,2022 Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendaji wa Shirika hilo huku akieleza kuwa  lilianzishwa mwaka 1962 likiwa na jukumu la kuwezesha ujenzi wa nyumba na majengo mengine kwa matumizi mbalimbali hususan makazi, Ofisi na biashara. 

Sambamba na hayo ameeleza kuwa NHC itatumia kiasi cha dola za Marekani Milioni 200 sawa na jumla ya shilingi Bilioni 466 za Tanzania Kutekeleza Mpango wa ujenzi wa nyumba 5000 za gharama ya kati na chini ujulikanao kama Samia Housing Scheme(SHS) ikiwa ni ishara ya kuenzi na kutambua mchango wake Kwa watanzania.

Amefafanua kuwa mradi huo wa SHS unatarajiwa kutoa ajira 26,400 kwa watanzania ambapo ajira za moja kwa moja 17,600 na zisizo za moja kwa moja 8,800.

"Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na tunatamani watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo na asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa Dar esSalaam, na asilimia 20 zitajengwa Dodoma huku mikoa mingine ikijengwa kwa  asilimia 30,"amesema 

Meneja huyo amesema nyumba hizo zitaanza kujengwa mwezi Septemba eneo la Kawe Dar es Salaam kutajengwa nyumba 500 na Medeli Jijini Dodoma nyumba100 na  Mradi huu utatekelezwa kwa awamu na kutarajiwa kukamilika  mwaka 2025.

Katika kutekeleza vipaumbele vingine Saguya ameeleza kuwa NHC itakamilisha  ujenzi wa Mradi wa Morocco square ambao ujenzi upo kwenye hatua ya uboreshaji wa mandhari (landscaping) na ufungaji wa lifti na viyoyozi kazi ambazo hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu zitakamilika. 

Aidha amesema  sambamba na ujenzi huo, Shirika litaendelea na kukamilisha miradi ya Kawe 711 na Golden Premier Residence (GPR) iliyopo Kawe.

"NHC tukiwa na dhamana ya ujenzi tutaanzisha miradi mingine ya ujenzi wa majengo ya biashara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bukoba, Mwanza, Dodoma, Kahama, Morogoro, Masasi na Lindi"amefafanua

Amesema pia NHC itaendelea na utekelezaji wa miradi ya ukandarasi ikiwemo ujenzi wa Majengo ya Ofisi za Wizara nane  Jijini Dodoma, wenye gharama ya Shilingi Bilioni 186 na kutarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 na ujenzi wa Jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ujenzi wa majengo matano  ya  Wakala wa Ununuzi wa Serikali (GPSA), ujenzi wa jengo la TANZANITE Mirerani, ujenzi  wa Jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI) na miradi mingine itakayojitokeza.

"Hatutaishia hapo tutaendelea kutekeleza Mpango Maalum wa miaka mitano wa ukarabati wa nyumba za Shirika unaoishia mwaka 2027, kukarabati nyumba katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Tabora, Arusha, Kigoma, Morogoro, Lindi, Tanga, Mbeya, Mwanza, Singida na Kagera kwa gharama ya shilingi bilioni nane,"amesisitiza Saguya

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post