MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI  KUFANIKISHA SENSA 2022


Rais Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kuhusu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kutoka kwa Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano TCRA, Bi. Lucy Mbogoro kwenye banda ya TCRA katika maonyesho yaliyokuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kitaifa Arusha 3 Mei 2022. Kati- kati ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape M. Nnauye (Mb).

***********************

Uvumbuzi uliofanywa na Mamlaka ya Mawasliano Tanzania (TCRA) miaka 10 iliyopita unatumika kufanikisha sensa ya watu na makazi mwaka 2022. Makarani na wasimamizi wa shughuli hii wamewezeshwa kufika kwenye kaya husika kwa urahisi.

Mwaka 2012, TCRA ilikamilisha mfumo wa anwani za makazi na postikodi na kuuchapisha katika gazeti la Serikali namba 220 la tarehe 22 Juni mwaka huo. Ulikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa katika kuwapatia Watanzania anwani za uhakika.

Mfumo wa anwani za makazi na postikodi umeondoa kero na usumbufu wa kuelekeza mtu nyumbani kwako kwa kumwambia: “ fuata barabara ya vumbi, kisha pinda kushoto baada ya kontena jekundu, kulia baada ya wanapopiga matofali, kushoto baada ya kibanda cha mkaa na utaona nyumba yenye paa la bluu mbele ya meza za mamalishe”. Vitu hivyo vikihamishwa na watu hao wakihama itabidi kutoa maelekezo upya.

Mfumo wa anwani za makazi unatambua mtu anapoishi kwa namba ya nyumba na jina la barabara au mtaa. Mfano: Kimara Baruti, Barabara ya Sofia Kawawa, nyumba namba 24.

Pamoja na kurahisisha kufikiwa kwa maeneo mengi kwa ajili ya huduma mbalimbali, mfumo wa anwani za makazi unarahisha kutambulika kwa nyumba na majengo; mambo ambayo ni muhimu kwenye kupanga na kusimamia mipango mahsusi ya kutoa huduma kwa wananchi.

Mfumo huo pia unarahisisha utoaji wa huduma za dharura kama vile uokoaji na kukabiliana na maafa. Hebu fikiria adha ya zimamoto au gari la huduma za wagonjwa ( ambulensi) kufika makazi ya mtu aliyekuwa anaelekeza nyumbani kwake kwa kutumia vitu vinavyohamishika.

Mfumo unaongeza ufanisi katika usimamizi wa makazi ya watu na unarahisisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi kwa malengo mbali mbali; kama haya ya sensa.

Ni mfumo ambao uzinduzi wake ulimhusisha Rais wa Awamu ya Nne ya Uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Mwanamfalme wa Uingereza, Prince Charles.

Miaka 10 baadae, tarehe 8 Februari 2022, Rais wa awamu ya sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliuongezea nguvu alipoitisha kikao mahsusi cha watendaji wakuu wa serikali na wakuu wa mikoa mjini Dodoma na kuagiza kwamba mfumo wa kuweka majina ya utambuzi wa barabara na namba kwenye nyumba nchini kote ukamilike kabla ya sesa ya Agosti, ambayo sasa inaendelea.

Mara nyingi watanzania wanapotakiwa kujaza anwani zao kwenye fomu wanaweka anwani ya posta; na nying ni za taasisi. Hii haina tija, kwani nchi nzima ina masanduku ya posta ambayo hayafiki laki mbili (200,000) na mengi hayatumiki, kutokana na mwelekeo wa kupungua kwa barua zinazopitia pota kutokana na maendeleo ya teknolojia ambayo yamewezesha kuwepo njia za mawasiliano rahisi na zenye ufanisi zaidi.

Rais alielekeza kwamba mfumo wa anwani na makazi utekelezwe kama ‘operesheni’ ambayo aliita ‘Operesheni Anwani za Makazi. Wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziliagizwa kuutekeleza chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Utekelezaji wa Operesheni hiyo ulianza kwa kuunda prpgramu tumizi ya mfumo kukusanya taarifa za baabara, mitaa, njia na makazi. Vilevile kulifanyika mfunzo ya kuongeza uelewa wa viongozi ngazi za mikoa, halmashauri na serikali za mitaa kuhudu mfumo wa anwani za makazi na posta.

Kila halmashauri iliandaa mpango wa utekelezaji na kutoa majina ya barabara na mitaa na namba za nyumba.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape M. Nnauye amesema wizara imetenga shilingi bilioni 40 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kuendelea na uboreshaji wa mfumo huo.

Shughuli hizo ni pamoja na kuhakiki miundombinu iliyowekwa wakati wa Operesheni Anwani za Makazi ili kuhakikisha kuwa viwango vimezingatiwa.

Kumekuwepo malalamiko ya wadau kuhusu ubora wa nguzo zilizowekwa kwenye barabara na mitaa, sarufi ya majina yaliyowekwa na mahali nguzo ziliposimikwa. Haya, na mengine yaliyojitokeza, yatarekebishwa; amesisitiza Mhe. Nnauye

Wizara pia itahakiki taarifa zilizokusanywa kwenye Operesheni, itaboresha kanzidata na programu tumizi ya Mfumo na itaendelea kuunganisha Mfumo huu na Mifumo mingine ya kutoa huduma za kijamii. Kompyuta mbili zenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi data zitanunuliwa.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni kutoa elimu kwa umma; makundi maalum ya kijamii kuhusu manufaa na matumizi sahihi ya Mfumo na kujengea uwezo taasisi za umma na binafsi kutoa huduma kupitia Mfumo.

Sheria ndogo zitatungwa kuwezesha ujenzi na matumizi ya Mfumo. Sheria ya Mawasil;iano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) itapitiwa upya pamoja na kanuni zake ili kuleta ufanisi katika matumizi ya Mfumo wa anwani na makazi.

Shughuli nyingine ni kuandaa mwongozo ya namna mpya ya kufanya biashara kwa kutumia Mfumo.

Mkakati wa usimamizi, uendeshaji na uendelezaji wa Mfumo utawekwa. Aidha ufuatiliaji ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wake pia vitafanyika.

Mfumo wa anwani za makazi unaenda sambamba na mfumo postikodi, ambazo zinajulikana pia kama simbo za posta. Hizi ni mfumo maalum wa alama, tarakimu na herufi inayotambulisha eneo au mahali mtu anapoishi au kufanyia shughuli zake.

Tanzania inatumia mfumo wa namba na herufi na ambao una tarakimu tano. Namba zote tano zinaonyesha kata; wilaya, mkoa na kanda.

Postikodi za sehemu yoyote Tanzania zinaweza kupatikana kupitia simu ya mkononi, kwa kutumia menu kwenye simu. Bofya ∗152 ∗ 00# na fuata maelekezo. Pia zinapatikana kwenye tovuti ya:www.tanzaniapostcode.com.

Anwani za makazi na mfumo wa postikodi ni muhimu katika uchumi wa kidijitali, hasa kwenye biashara mtandao na ufikishaji wa huduma za kielektroniki. Vitakuwa kitovu cha utoaji wa huduma za biashara mtandao, ambalo ni mojawapo la lengo ma mradi wa Tanzania ya kidijitali.

Kwenye hili, Tanzania inatakiwa kuonyesha njia; kwani nchi yetu inaongoza Kamati ya Huduma za Posta na Biashara Mtandao ya Umoja wa Posta Duniani, wenye makao yake makuu Berne, Uswisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post