MASELE ASHINDA KWA KISHINDO KURA ZA MKUTANO MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA MJINI

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Masele ameshinda kwa kura 69 kati ya kura 85 katika uchaguzi wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mjini uliofanyika leo Jumatano Agosti 3,2022.


Kwa Mujibu wa Mwenyekiti Msaidizi wa Uchaguzi wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu amesema Stephen Masele ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP) ameongoza kwa kura 69 kati ya kura 85 katika kundi la wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ambalo linatakiwa kuwa na wawakilishi watano.

Katika uchaguzi huo wa ndani ya chama unaendelea ukihusisha uchaguzi wa Mwenyekiti, Katibu, Katibu wa Siasa na uenezi na wajumbe watano wa halmashauri kuu ya Kata , Wajumbe watano wa mkutano Mkuu wa wilaya na mjumbe mmoja wa mkutano mkuu wa mkoa, ambapo George Mwandu Mwele amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM kata ya Ngokolo.

Wajumbe wa mkutano huo wamesema wana imani kubwa na Mhe. Masele ambaye amekuwa akijitoa sana katika kukisaidia chama kwa michango mbalimbali.

Mhe. Masele pamoja na kwamba sio mbunge tena lakini amekuwa karibu na watu na kuwasaidia shida mbalimbali na kujitoa sana kwa ajili ya chama”, amenukuliwa akisema Mjumbe Omari Malula.

Naye Mjumbe mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jaffari ambaye ni katibu wa tawi la Mshikamano amesema “Masele ni mtu wa watu, mnyenyekevu na ana heshima sana, ana heshimu watu bila kujali hali zao za kimaisha ni kiongozi aliyepikwa akaiva na Chama Cha Mapinduzi. Ni zao halisi la CCM”.

"Masele kama ni kijana msomi mwenye uelewa mkubwa sana, ni Hazina kwa mkoa wa shinyanga na taifa kwa ujumla, kama ulivyoona wajumbe wote wamemchagua kwa kishindo kwa kuwa wanampenda ni kipenzi chao”,amesema mjumbe mwingine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post