DC MBONEKO ATINGA NYUMBANI KWA ALIYEGOMA KUHESABIWA SHINYANGA...AREJESHA FURAHA YAKE

 

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (kulia) akifurahia jambo na Mariam Paulo Gitula mara baada ya kumaliza kuhesabiwa Sensa.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amefanikisha mtu mwenye ulemavu kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi Mariam Paulo Gitula mkazi wa Mtaa wa Busulwa Kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga, baada ya kuwagomea Makarani kwa madai hajaingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini TASAF.

Mboneko amefanikisha zoezi hilo leo Agosti 28, 2022, ambapo mlemavu huyo aligoma tangu jana Agosti 27 kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi.

Amesema baada ya kufika kwenye Kaya hiyo, amezungumza na mtu huyo mwenye ulemavu na kumuahidi kuwa ataingizwa kwenye Mpango huo wa TASAF kwa sababu vigezo anavyo, huku akimkatia na Bima ya Afya CHF iliyoboreshwa ambayo itamsaidia katika matibabu.

“Tuliagiza Makarani watakapokutana na changamoto yoyote ile ambayo ipo juu ya uwezo wao watupe taarifa, na leo tumepata taarifa ya mtu huyu mwenye ulemavu kugoma kuhesabiwa Sensa hadi aingizwe kwenye TASAF, na nimefika hapa suala hili nimelimaliza na yayari amehesabiwa,”amesema Mboneko.

“Mbali na kumuahidi kuingizwa kwenye Mpango wa TASAF ambapo tayari nimeshatoa maelekezo, pia nimemkatia na Bima ya Afya CHF iliyoboreshwa, ili awe anapata matibabu bure na watoto wake wawili ,”ameongeza.

Aidha, amesema zoezi hilo la Sensa katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga linaendelea vizuri, na hadi sasa limefika asilimia 100.

Naye Karani Mweya Wambura Sauti, amesema baada ya kufika kwenye Kaya ya Mtu huyo Mwenye ulemavu jana aligoma kuhesabiwa akidai kuwa hajaingizwa kwenye TASAF, na baada ya kugoma ndipo ikabidi waombe msaada ngazi za juu na kufanikisha kumwandikisha leo.

Kwa upande wake mtu huyo mwenye ulemavu Mariam Paulo Gitula, amesema kuwa aligoma kuhesabiwa hadi pale atakapoingizwa kwenye mpango wa TASAF, lakini baada ya kufika Mkuu wa wilaya Jasinta Mboneko na kumuahidi kuwa ataingizwa ndipo akakubali kuhesabiwa, huku akisisitiza kuwa ahadi hiyo iwe ya kweli kwa sababu anaishi maisha magumu.

Aidha, zoezi la kuhesabu Sensa ya watu na makazi hapa nchini lilianza Agosti 23 mwaka huu, na linatarajiwa kukoma hapo kesho Agosti 29.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza namna alivyotatua mgomo wa mtu mwenye ulemavu kugoma kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi, akida hahajingizwa kwenye TASAF na wakati anaisha maisha magumu.

Karani Mweya Wambura Sauti, akielezea ugumu aliokutana nao kwenye Kaya hiyo ya mtu mwenye ulemavu na kugoma kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi.

Mtu mwenye ulemavu Mariam Paulo Gitula, akielezea madai yake ya kutoingizwa kwenye TASAF ndipo akagoma kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi, na baada ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga kuzungumza naye ndipo akakubali kuhesabiwa.

Karani wa Sensa ya watu na Makazi Mweya Wambura Sauti, akiingiza Taarifa na Mtu mwenye ulemavu Mariam Paulo Gitula, (wapili kutoka kulia), mara baada ya tatizo lake kumalizwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (wa kwanza kushoto) la kudai kuwa hadi aingizwe kwenye TASAF ndipo ahesabiwe Sensa, (kulia) ni jirani yake Ruth Edwin.

Zoezi la kuingiza taarifa likiendelea.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (kulia) akifurahia jambo na mtu mwenye ulemavu Mariam Paulo Gitula mara baada ya kumaliza kuhesabiwa Sensa.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (kushoto) akifurahia jambo na mtu mwenye ulemavu Mariam Paulo Gitula mara baada ya kumaliza kuhesabiwa Sensa.

Picha ya pamoja ikipigwa mara baada ya zoezi la kuhesabu Sensa kwenye Kaya ya mtu mwenye ulemavu Mariam Pualo Gitula kukubali kuhesabiwa Sensa, kulia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Busulwa Anthony Mashishanga, akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.

Makarani na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwa kwenye Kaya ya mtu mwenye ulemavu Mariam Paulo Gitula ambaye awali aligoma kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post