Mchanganyiko wa pombe yenye sumu iliyoua watu 14 kaskazini-magharibi mwa Uganda imewaacha wengine wakiwa vipofu, daktari mmoja ameliambia gazeti la Daily Monitor la nchi hiyo.
Waathiriwa wote wanaaminika kutumia pombe kali iliyotengenezwa nchini humo inayoitwa City 5 Pineapple Flavored Gin mwishoni mwa juma katika wilaya ya Madi-Okollo.“
Hawa watu sasa wamepoteza uwezo wa kuona, baadhi yao kwa kiasi, huku wengine wakiwa vipofu kabisa. Kwa kiasi ina maana bado wanaweza kuwa na uwezo wa kuona lakini sio vizuri kama walivyokuwa hapo awali” alisema Dkt Onesmus Misoa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Arua.
Polisi wamewakamata watu wanne kutokana na tukio hilo huku mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza pombe hiyo akiwa mafichoni.
Chanzo - BBC Swahili