JAMAA AWACHOMA KISU WANAWAKE WAWILI KISA HAWAMUUNGI MKONO BABA YAKE ANAYESAKA UBUNGE


Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 17 anazuiliwa na polisi eneo la Gilgil katika Kaunti ya Nakuru nchini Kenya baada ya kuwadunga kwa kisu mara kadhaa wanawake wawili kwa madai ya kukataa kuunga mkono azma ya ubunge ya babake ambaye ni mwanasiasa mashuhuri kaunti ya Nakuru.


Jane Kibe mwenye umri wa miaka 48 na Peris Wanjiru mwenye miaka 35 kwa sasa wanaendelea kupata afueni katika Hospitali ya Nakuru War Memorial baada ya kudungwa mara 18 na 19 mtawalia kufuatia kisa hicho kilichotokea eneo la Teachers Estate, Gilgil.


Kibe anasema kuwa alishangazwa mvulana huyo ambaye ni rafiki wa mvulana wa Wanjiru, alipoingia katika chumba chake cha kulala na kuchomoa kisu akiapa kuwa angemuua. 

“Sikuelewa jinsi gani nilivyomkosea. Alinisukuma kwa kitanda na akaanza kunidunga kwa kisu. Alinituhumu kukosa kuunga mkono babaake ambaye ni mgombea wa ubunge,” Kibe alisema kwa mujibu wa gazeti la the Standard.


Kilio cha Kibe cha kutaka msaada kilimvutia Wanjiru ambaye alikuwa bafuni kwa wakati huo na alipojaribu kuingilia mshukiwa alibadili ngoma kwake.

 “Nilianza kuitisha msaada. Alinidunga kwa mikono, mapanga na mgongo. Madaktari waliniambia kuwa moja wa jeraha lilikosa kidogo tu kufikia moyo huku jingine likijeruhi pafu langu la kushoto kidogo,” Kibe amenukuliwa. 

Akithibitisha kis hicho, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nakuru Peter Mwanzo aliambia waandishi wa habari kuwa uchunguzi unaendelea na kijana huyo anasalia korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani kwa jaribio la kutekeleza mauaji.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post