WATATU WA FAMILIA MOJA WAFARIKI KWA KUGONGWA NA GARI ARUSHA WAKIPELEKA MTOTO HOSPITALI

Watu watatu wa familia moja akiwemo mtoto mdogo,wakazi wa kata ya Terat  katika jiji la Arusha,wamepoteza Maisha papo hapo  kwa ajali baada ya kugongwa na gari wakitoka hospitalini wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki.


Tukio hilo la kusikitisha limetokea usiku wa kuamkia leo katika barabara ya bypass katika jiji la Arusha wakati marehemu wakitoka kumpeleka hospitalini, mtoto Ebenezer Mollel mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu aliyekuwa ameandikiwa sindano za masaa.

Wengine waliofariki dunia ni pamoja na mama wa mtoto ,Neema Mollel(27) pamoja na mdogo wake ,Agustino Mollel (24) ambaye alikuwa dereva wa pikipiki .

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo,John Mushi marehemu hao walipoteza maisha eneo la tukio baada ya kupata majeraha makubwa na  kuvuja damu nyingi.

Alisema walishuhudia miili ya marehemu hao wakiwa wamevunjika na kusagika mikono na miguu huku mtoto na dereva  wakipasuka kichwa  na kusagika.

Naye kaka wa marehemu Daud Mollel alisema kuwa marehemu waligongwa kwa nyuma wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki na gari ambalo halikujulikana baada ya kutosimama katika eneo la Karvati ,Terat. 

Alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa juu ya ajali hiyo alifika eneo la tukio na kushuhudia miili ya marehemu wakiwa ikiwa na majeraha makubwa sehemu mbalimbali za miili yao.

"Marehemu walitoka nyumbani Terat majira ya saa 10 usiku kwenda hospitali  ya Murieti  baada ya mtoto (marehemu)kuandikiwa sindano za masaa,wakati wakirudi majira ya saa kumi na moja kasoro ndipo walipogongwa na gari  kwa nyuma na kufariki dunia"alisema

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa bado wanafanya uchunguzi kujua chanzo cha tukio hilo.

Kamanda alisema kuwa gari lililohusika na tukio hilo halikuweza kupatikana na polisi wanaendelea na uchunguzi ili kumtia mbaroni dereva wa gari hilo ambaye alitoweka mara baada ya ajali hiyo.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha maiti katika kituo cha afya  cha Murieti kusubiri taratibu wa uchunguzi .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments