RUWASA KUTEKELEZA MIRADI 1,029 KUONDOA UHABA WA MAJI

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi  Clement Kivegelo akizungumza na Waandishi wa habari leo Julai 19,2022 Jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa, DODOMA 

KWA mwaka wa fedha  2022/23 Wakala wa Maji Vjijini (RUWASA) umepanga kutekeleza jumla ya miradi 1,029 huku kati ya miradi hiyo 381 ni mipya na miradi 648 ile ambayo utekelezaji wake unaendelea kutoka mwaka wa fedha uliopita.

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi  Clement Kivegalo amesema hayo leo Julai 19,2022Jijini Dodoma  wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wake,utekelezaji,mwelekeo na mafanikio yake na kueleza kuwa  jumla ya kiasi cha Shilingi bilioni 387.7 imeidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. 

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo, kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kuongezeka kwa wastani wa asilimia sita na kwamba utekelezaji wa shughuli zake unaongozwa na Mpango Mkakati wa miaka mitano, yaani 2020/2021 hadi 2024/2025 utakaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini hadi kufikia kiwango kisichopungua asilimia 85 kwa mwaka 2025.

Akieleza hali ya upatikanaji wa maji kabla na baada ya kuundwa RUWASA,Mhandisi Kivegalo amesema,wakati wa kuanzishwa kwake, RUWASA ilirithi jumla ya skimu za maji 1,379 zilizokuwa zimekamilika na kulikuwa na miradi 632 ya ujenzi wa skimu za usambazaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini na kueleza kuwa kati ya skimu hizo zilizokuwa zimekamilika 177 zilikuwa hazitoi huduma ya maji kwa wananchi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukauka kwa vyanzo vya maji.

Amefafanua kuwa mwezi Julai 2019 upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ulikuwa ni wastani wa asilimia 64.8 ambapo pamoja na kiwango hicho cha upatikanaji wa maji, kwa ujumla, hali ya huduma ya maji vijijini haikuwa ya kuridhisha. 

Sambamba na hayo alisema ujenzi wa miradi ulikuwa ukichukua muda mrefu na kwamba hata miradi iliyokuwa ikikamilika na kuzinduliwa, ilidumu muda mfupi na kusababisha wananchi wa vijijini kuendelea na adha ya maji huku akieleza kuwa miradi hiyo ilikuwa ikijengwa kwa gharama kubwa ikilinganishwa na uhalisia wa soko.

Mhandisi hiyo pia amesema pamoja na utekelezaji wa mpango wa bajeti 2021/2022, kuliibuka pia uhitaji wa mradi wa maji kwa wananchi wa Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni ambacho  wananchi kutoka Ngorongoro walihamia kwa hiari.

Kutokana na hayo ameeleza kuwa RUWASA inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji hicho, ambapo mpango wa utekelezaji uligawanywa katika awamu mbili (awamu ya muda mfupi na awamu ya muda mrefu).

"Awamu ya muda mfupi imekamilika na vituo vya kuchotea maji 12 vimeshaanza kutoa huduma ya maji, awamu ya pili imefikia asilimia 70 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2022,kukamilika kwa awamu hiyo kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 17,000 pamoja na mifugo yao ,

Aidha hali hiyo itapelekea idadi ya vituo vya maji kuongezeka kutoka 12 hadi kufikia vituo vya kuchotea maji 30 kwa matumizi ya binadamu na vituo 3 vya kunyweshea maji mifugo,"amesisitiza 

Sambamba na hayo ameweka wazi kuwa Wakala huo  unafanya jitihada kuboresha huduma ya maji katika Kijiji cha Msomera na kwamba Serikali kupitia RUWASA inaendelea na ujenzi wa bwawa la maji kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.99 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 15.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post