ADAIWA KUMUUA BABA NA MAMA TUHUMA ZA KUWA WANAMROGA


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa.

**
Na Mary Mosha Nipashe
JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia Jonas Mushi (26) Mkazi wa Manushi wilayani Moshi kwa tuhuma za mauaji ya Baba yake mkubwa pamoja na mkewe kwa kuwacharanga na panga kutoka na tuhuma za kuwa wanamroga.


Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema tukio hilo limetokea Julai 19 mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika Kijiji cha Manushi kati.


Kamanda Maigwa, alisema kuwa awali kabla ya tukio hilo mtuhumiwa alifika nyumbani kwa marehemu na kuingia ndani na kuchukua panga na kuanza kumshambulia baba yake mkubwa aitwae Mariki Mushi.


Wakati akiendelea kumshambulia ndipo mke wa marehemu aitwae Felister Mushi alipoingilia kwa lengo la kumsaidia mumewe asishambuliwe ndipo mtuhumiwa alimgeukia mama yake mkubwa na kuanza kumshambulia.


"Mtuhumiwa aliendelea kuwashambulia kwa kuwakatakata na panga mpaka kuhakikisha wote wanapoteza maisha kwani aliwakata maeneo mbalimbali ya mwili" alisema


Aliongeza kuwa, chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina kwani mtuhumiwa anawatuhumu marehemu kuwa ni wachawi na wamekuwa wakimroga. Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments