DUWASA YATAJA MIKAKATI YAKE KUMALIZA KERO YA MAJI

Mkurugenzi wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli na mwelekeo wa mamlaka hiyo  kwa mwaka wa fedha 2022/23 leo Julai 25,2022 Jijiñi Dodoma 

Na, Dotto Kwilasa, DODOMA 

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA) imetenga kiasi cha shilingi bilioni 9.5 kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwajili ya ukarabati na uchimbaji wa Visima pembezoni mwa Jiji la Dodoma.

Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo (DUWASA)Mhandisi Aron Joseph amesema hayo  leo Julai 25,2022 Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za DUWASA na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23

Amevitaja vyanzo ambavyo vitanufaika na fedha hizo kuwa ni pamoja na vile  vilivyopo maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Dodoma kwa kuhusisha  Zuzu, Ihumwa, Mpunguzi, Nala, Michese, Zinje na Nzuguni. 

Amesema kwa sasa Jiji la Dodoma lina takwimu za idadi ya Wakazi 500,000 ambao wanapata maji safi ni asilimia 82,
mahitaji ya maji ni lita milioni 133 kwa siku hii ni kwa mwaka 2022 na yataongezeka hadi lita milioni 204 kwa siku hadi ifikapo mwaka  2036.

Ameongoza kuwa uwezo wa kuzalisha maji ni lita milioni 67.1 kwa siku kituo cha Makutupola pekee ni  lita milioni 61.5,huku vituo vingine vikizalisha lita milioni 5.6 sawa na asilimia 50ya mahitaji ambapo muda wa kutoa huduma ni wastani wa saa 10 kwa siku,"amefafanua Mha.Joseph.

"Lengo letu ni kuondoa kabisa kero ya Maji,tuna mipango inayopewa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2022/23 , kwa  upande wa maji safi DUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji tunaendelea na utafiti wa namna bora ya kuendana na kasi ya mahitaji, kwa kubuni mbinu mbalimbali za utatuzi wa changamoto ya uhaba wa majisafi na uondoshaji Majitaka kwa kuanzisha utekelezaji wa mipango ya dharura, muda mfupi, kati na mrefu ili kuongeza kiasi cha upatikanaji wa maji kwa ajili ya Jiji la Dodoma,"amesema.

Mkurugenzi huyo pia ameeleza  Mpango mwingine kuwa ni wa Dharura na Muda Mfupi,Ujenzi wa Mradi wa kutoa maji Bwawa la Mtera ambapo Chanzo kipo tayari ambacho kitakamilishwa kati ya miaka 2 hadi 2.5 huku Benki ya Dunia ikiwa tayari kufadhili gharama ya Mradi ni Dola milioni 140 sawa na bilioni 326 za Tanzania.

"Mradi huu utaongeza maji lita milioni 130 kwa siku pia utaongeza mtandao wa usambazaji maji katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na kuondoa migao ya mamaji,"amefafanua

Kwa upande wa  fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19,Mha.Joseph amesema DUWASA kupitia Wizara ya Maji ilipokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 huku mradi wa Ntyuka Chimalaa ukikamilika kwa asilimia 100,Bahi town kwa asilimia 100 
na uchimbaji wa visima 6 kwa asilimia 100 huku jumla ya wanufaika wakiwa 40,000.

"Kuna mpango wa muda wa Kati na Mrefu ambao ni ujenzi wa Bwawa la Farkwa ukiwa na muda wa mradi miaka 5 hadi 6 na 
Ongezeko la maji mita milioni 128 kwa siku gharama ya mradi ikiwa Dola milioni 135.8 sawa na shilingi bilioni 312.08 za Tanzania,

"Tarehe 16/05/2022 Serikali ya Tanzania ilisaini financial agreement na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ya Dola mil. 125.3 (shilingi Bilioni 289) kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa pamoja na Chujio (treatment plant) na mpaka sasa tayari Mhandisi Mshauri amepatikana na anatarajiwa kusaini mkataba mwezi Agosti mwaka huu,"ameeleza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments