BILIONI 11.9 KUTUMIKA KWENYE MAPAMBANO DHIDI YA DAWA


Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na uratibu George Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 29,2022 Jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa, DODOMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George simbachawene ameeleza vipaumbele vya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2022/23 huku akisema Mamlaka ya kupambana na kudhibiti Dawa za Kulevya imeidhinishiwa jumla ya bilioni 11.9 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.


Simbachawene amesema hayo leo Julai 29,2022 wakati akiongea na Waandishi wa habari na kufafanua kuwa fedha hizo ni ongezeko la asilimia 28.8 ikilinganisha na kiasi cha shilingi bilion 8.5 kilichoidhinishwa mwaka wa fedha 2021/22.


Ameongeza kuwa ongezeko hilo la bajeti ya mamlaka hiyo litaendelea kuimarisha udhibiti wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini, kuimarisha ushirikiano miongoni mwa vyombo vinavyojihusisha na udhibiti wa dawa za kulevya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia zinazohusu biashara haramu ya dawa kulevya.


Kuhusu mapambano dhidi ya Virusi vya Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) Waziri Simbachawene amesema katika mwaka wa fedha 2022/23,Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania iliidhinishiwa na Bunge shilingi bilion 14.9 kufafanua kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilion 2.9 ni kwa ajili ya matumizi ya Kawaida na sh.bilion 12 ni kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.


“Shughuli zitakazotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 ni pamoja na kuratibu upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI kwenye Mikoa ya kipaumbele ikiwemo Iringa, Kagera, Katavi, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Dodoma, Geita, Tabora na Songwe pamoja na kuweka kipaumbele katika kuzuia maambukizi ya VVU kwa vijana wa miaka 15 -24,”amesema

Katika hatua nyingine Waziri huyo amesema katika kuhakikisha serikali inaendelea kukuza Demokrasia imeendelea kufanya jitahada mbalimbali zenye lengo la kukuza Demokransia nchini ikiwemo kuhakiki maeneo ya uchaguzi na vituo vya kuandikishia wapiga kura kwa kuboresha mifumo ya menejimenti ya uchaguzi,kuratibu na kusimamia uendeshaji wa chaguzi ndogo.


"Jitihada nyingine ni kuendesha vikao na wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa,kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi,kuimarisha taratibu za upatikanaji na uwekaji wa takwimu kwa kuandaa mfumo maalum, kuboresha sheria za uchaguzi na kuandaa vituo vya kuandikishia wapiga kura,"amesema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post