MKUNGA ALIYEZALISHA MAMA WAJAWAZITO NJE YA GETI LA ZAHANATI YA KASHAI BUKOBA AISHUKURU TANESCO KUMWEKEA UMEME


Bi. Leokadia Samwel Byabato pamoja na Diwani wa kata ya Kashai Mh. Ramadhan Kambuga kushoto pamoja na Afisa mahusiano na huduma kwa wateja wa Shirika la Tanesco Bw. Samwel Mandari (wa pili kulia).
Wapili kulia ni Afisa mahusiano na huduma kwa wateja wa Shirika la Tanesco Bw. Samwel Mandari akimkabidhi Bi. Leokadia kifaa cha kuwekea Luku
Mfanyakazi wa Tanesco akiunganisha  umeme katika nyumba Mpya ya Bi. Leokadia ambaye alisaidia kuzalisha akina mama wajawazito nje ya geti la Zahanati ya Kashai
Na Mbuke Shilagi Kagera.

Mkunga Leokadia Samwel aliyezalisha akina mama wajawazito nje ya geti la Zahanati ya Kashai baada ya wahudumu kugoma kuwafungulia geti mnamo Julai mosi 2022 majira ya saa 10 alfajiri, ameishukuru Tanesco kwa kumuwekea umeme katika nyumba yake ikiwa ni moja ya shukrani ya kuokoa maisha ya mama wajawazito hao.

Akizungumza na vyombo vya habari Bi. Leokadia amesema kuwa Shirika la umeme Tanesco kwa kumuwekea umeme imekuwa ni jambo furaha sana kwani ataondokana na kutumia kibatari  kama alivyokuwa akiishi hapo mwanzo.

"Pia namshukuru Diwani wa kata ya Kashai Mh. Ramadhan Kambuga kwa kuwa pamoja na mimi toka usiku ule wa kuzalisha wale wamama wajawazito mpaka sasa ambapo watu mbalimbali pamoja na viongozi ambao wamekuwa wakitoa msaada kwangu bado tuko pamoja lakini pia namshukuru Naibu Waziri wa Nishati Mh. Steven Byabato alietekeleza jambo hili kwa kuniwekea umeme kwani nilikuwa natumia kibatari lakini sasa nakipa kwaheri kibatari", amesema Bi. Leokadia.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kashai Mh. Ramadhan Kambuga amewashukuru watu wote pamoja na viongozi mbalimbali ambao wameendelea kumchangia Bi. Leokadia ikiwa ni kama shukrani ya kuweza kuwazalisha wamama wawili nje ya geti la Zahanati kutokana na makazi ya mama huyo mkunga kutokuwa mazuri.

"Niseme kama Diwani wa Kashai tunaendelea kuwashukuru sana watu wote na tuendelee kuiga mfano wa Manispaa yetu ya Bukoba tunao wahitaji wengi lakini wahitaji wanazidiana huyu mama kitendo cha kuokoa wamama wawili na watoto wao wawili ni jambo ambalo kila mtu alitakiwa kulipongeza na kuliunga mkono", amesema Mh. Kambuga.


Naye Afisa mahusiano na huduma kwa wateja wa Shirika la Umeme Tanesco Bw. Samwel Mandari amesema kuwa ni utaratibu wa kawaida kabisa kama Shirika kuweza kuchangia kwenye masuala ya kijamii.

"Na leo nafurahi kabisa tumekuja kumuwekea umeme bibi yetu huyu ambaye alifanya tendo la kishujaa kwa kuwasaidia akina mama wawili kujifungua salama ambao  walipata changamoto katika Zahanati ya Kashai" ,amesema Mandari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post