NGARA YAPATA HATI SAFI, RC AWATAKA MADIWANI KUSIMAMIA MAPATO


Mkuu wa Wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Halmashauri ya wilaya ya Ngara Mkoani Kagera imepata hati safi kwa miaka mitano mfurulizo ikiwa imeshika nafasi ya tatu kati ya halmashauri nane za mkoa huo kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Katika taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) iliyosomwa kwenye baraza maalumu la kujadili taarifa hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Solomon Kimilike ameeleza kuwa kufanikiwa kwao kunatokana na ushirikiano uliopo baina ya madiwani, ofisi ya mkuu wa wilaya na menejimenti ya halmashauri hiyo.


Ameongeza kuwa ili waweze kuendelea kufanya vizuri, ushirikiano huu wanatakiwa kuudumisha hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoletwa kwenye maeneo yao.

Akiongea kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja jenerali Charles Mbuge, Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi ameipongeza halmashauri hiyo chini ya mkurugenzi kwa kuendelea kusimamia vyema vyanzo vya mapato ya ndani hali iliyowapeekea kupata hati safi.


Kanali Kahabi amewataka madiwani kuongeza ukaribu na usimamizi wa miradi ya maendeleo inayoletwa kwenye kata zao ili kuweza kutekelezwa kwa ufanisi na kutoa huduma kwa wananchi kwa muda uliopangwa.


Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Wilbard Bambala amewataka madiwani kuwa mstari wa mbele katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ambapo ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kufikia mwezi mei halmashauri ilikuwa imekusanya zaidi ya asilimia 150 ya lengo lake.


Baraza maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara la kujadili hoja za Mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) kwa Mwaka wa fedha 2020/2021.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments