TANESCO NI-KONEKT YAIBUA SHANGWE CHATO

Meneja wa Tanesco wilaya ya Chato ukitoka maelezo ya namna ya kutumia njia Bora ya kidijitali ya Ni-konekt
Wafanyakazi na mafundi wa Tanesco chato wakiwa kazini

Na Daniel Limbe, Chato

WAKAZI wa kata ya Bwina wilayani Chato mkoani Geita, wamepata fura kubwa baada ya shirika la umeme nchini (Tanesco) kuwaunganisha na huduma ya nishati hiyo majumbani mwao.


Shangwe,nderemo na vifijo vimeibuka leo Juni 7,2022 muda mfupi baada ya meneja wa Tanesco wilaya ya Chato,Emily Ntazimila, kuwasha umeme kwenye nyumba ya Getruda Mremwa,mkazi wa kijiji cha Zanzibar kata ya Bwina, ikiwa ni ishara ya wananchi hao kuanza kunufaika na nishati hiyo kwa mfumo wa kidijitali.



Akizungumza na wakazi hao, Meneja huyo amesema shirika la umeme nchini(Tanesco) limekuja na mpango mpya wa Ni-konekt ili kurahisisha huduma kwa wateja wake kwa kufanya maombi ya kuunganishiwa umeme pasipo kufika ofisi za Tanesco.



"Mpango huu unarahisisha sana maombi ya wateja wetu kupata umeme pasipo kuja ofisini...mteja wetu atalazimika kutumia simu yake ya mkononi, kompyuta mpakato au intanet badala ya kutumia gharama kubwa za kutufikia ofsini kwetu"amesema



Ofisa huduma kwa wateja Tanesco wilaya ya Chato, Salma Mbwana, amedai kuwa huduma ya Ni-Konekt ina faida rukuki kwa wateja ikilinganishwa na awali ambapo wateja walipaswa kufika kwenye ofisi za Tanesco.



"Ni-Konekt inamrahisishia mteja kupata kwa urahisi zaidi, inaokoa muda, inaondoa kero za vishoka, inaongeza ufanisi wa kazi katika upatikanaji wa huduma na kwamba huduma hizi sasa zinapatikana kwa kutumia simu ya mkononi kwa kupiga alama ya *152*00# kisha unaendelea kupata maelekezo zaidi",amesema.



Hata hivyo amewataka wakazi wa wilaya ya chato kuchangamkia fursa hiyo ambayo imelenga kuondoa malalamiko ya awali ambapo wananchi walikuwa wakitapeliwa fedha zao na vishoka.



Kwa upande wake, Bi Mremwa, amelishukuru shirika la umeme nchini, kwa kumpatia haraka huduma ya umeme baada ya kufanya maombi jana juni 6 mwaka huu kabla ya leo kuwashiwa.



Akatumia fursa hiyo kuwasihi wananchi kutumia njia mpya ya kidijitali ya Ni-Konekt kufanya maombi ya kuunganishiwa umeme kwa kuwa ni bora na haraka zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments