NDONDO CUP KUANZA KUTIKISA DODOMA


    Na Dotto Kwilasa, DODOMA 

MARA baada ya Mashindano ya Ndondo Cup kufanyika kwa miaka 9 mfululizo  Jijini Dar es salaam sasa kwa mara ya kwanza ni zamu ya mashabiki wa Soka Mkoani Dodoma kuyashuhudia.

Mashindano hayo yametoa baadhi ya wachezaji ambao kwa sasa wanacheza Ligi kuu na Championship kama Kelvin Sabato ‘kiduku’ (Mtibwa Sugar) ,Iddi Nado (Azam) George Mpole (Geita),Anuary Jabir (Dodoma Jiji).

Akizungumza June 24,2022 wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, ulioshuhudiwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Kilimo,Antony Mavunde,Mratibu wa  Mashindano hayo hayo,Yahaya Mohammed  ‘Mkazuzu’  amesema jumla ya timu 16 zinatarajia kushiriki  mashindano hayo.

Amesema kwa Mkoa wa Dodoma bingwa anatarajia kuondoka na kitita cha Shmilioni 5 huku mshindi wa pili akijipatia Shmilioni 3 na kikundi bora cha ushangiliaji kikilamba Shmilioni moja.

“Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma ndio watasimamia kila kitu na ada itakuwa Sh200,000 kauli mbiu yetu ni twende pamoja hivyo ni lazima twende pamoja na vijana wa Dodoma,”amesema Mkazuzu.

Kwa upande wake Mavunde amewapongeza waandaaji wa mashindano hayo kwa kuleta fursa kwa vijana wa Dodoma kwani hiyo itakuwa ni fursa  kwa  baadhi ya timu kupata wachezaji kupitia mashindano hayo.

“Dodoma hatupendi kushindwa tumejipanga kwa hii fursa na naamini tutawashinda watu wa Dar es salaam,tunataka yawe mashindano endelevu kwa ajili ya timu zetu Dodoma Jiji na Fountain Gate kuvuna wachezaji,”amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (DOREFA) Majuto Msekela amesema wapo tayari kuandaa mashindano hayo kwa kuweka waamuzi ambao watatafsiri sheria vizuri pamoja na kutafuta viwanja ambavyo ni rafiki kwa kucheza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post