DKT. MAHERA AHIMIZA WATANZANIA KUHESABIWA

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt.Wilson Mahera Charles

Na Mwandishi Wetu, DODOMA


Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt.Wilson Mahera Charles amewataka watanzania kuwa tayari kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa ya watu na makazi litakayofanyika Agosti 23, 2022, nchini kote.

Wito huo ameutoa leo ofisini kwake jijini Dodoma na kusema kuwa zoezi la Sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwani hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutegemea takwimu za sensa kukadiria idadi ya wapiga kura wapya watakaoandikishwa pamoja na waliopoteza sifa za kuandikishwa. 

“Kimsingi wapiga kura au shughuli za uchaguzi kwa ujumla zina uhusiano mkubwa na takwimu zitokanazo na sensa, kwani katika sensa ndipo Tume inaweza kubainisha idadi ya watu itakayowaandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura,”amesema Dkt. Mahera na kuongeza:

“Nawahimiza watanzania wote kujitokeza kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi mwaka huu na kila mmoja kumhamasisha mwenzake kuhesabiwa.”

Amesisitiza kuwa ili Tume huyo ifanye shughuli zake vizuri ni lazima ipate takwimu sahihi za watu, makazi na kutambua makundi maalum ambayo ni ya wanawake, wazee, vijana na watu wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi ameongeza kuwa ," kutokana na sensa ya mwaka huu kufanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ambayo itawezesha kutambua idadi ya majengo ya umma na makazi ya watu, Tume tutatumia takwimu hizo, kuweka vituo vya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura,"amefafanua na kuongeza;

Sensa ya mwaka huu itafanyika kidijiti na itaweza kubainisha idadi ya majengo ya umma ambayo sisi huyatumia kuweka vituo vya kujiandikisha, lakini pia itatusaidia pia kuweka vituo hivyo kwa mujibu wa anuani za makazi ambazo pia sensa inakwenda kuzitambua rasmi,” amesema Dkt Mahera.

Dkt Mahera pia amesema Tume imekua ikipanga mipango yake kwa takwimu kuanzia ngazi ya kata lakini sasa kwa kuwa sensa inakwenda kuweka kumbukumbu hadi ngazi ya kitongoji, itaweza kupanga mipango yake kwa urahisi zaidi na matumizi ya teknolojia katika uchaguzi yataongezeka.

Sensa ya watu na makazi hufanyika kila baada ya miaka 10 na mara ya mwisho Sensa hiyo ilifanyika mwaka 2012 ambapo watanzania milioni 44,929 walihesabiwa. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments