CHUO CHA SERIKALI ZA MITAA HOMBOLO KIMEANDAA MPANGO WA KUWASAIDIA WANAFUNZI WALIOSHINDWA KUPATA UFAULU MZURI


Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano- LGTI  akiwaelekeza baadhi ya wanafunzi waliomaliza elimu ya Sekondari waliotembelea kwenye banda la maonyesho la chuo hicho kuhusu namna ya kujiunga na chuo hicho ikiwa ni moja ya nguzo  muhimu katika kuwajenga,kuwaimarisha na kuwapa ari ya kujiendeleza katika kozi mbalimbali.

Mhadhiri mwandamizi wa chuo cha Serikali za mitaa Hombolo Bundala Dodo akitoa maelekezo kwa mwananchi aliyetembelea banda la chuo hicho kuhusu namna wanavyoendesha kozi mbalimbali .

Na Dotto Kwilasa,DODOMA 

CHUO cha Serikali za Mitaa (LGTI),Hombolo-Dodoma kimesema kina mpango wa kutembelea shule za Sekondari nchi nzima kuona namna ya kuwaelimisha wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kushindwa kupata alama za kujiunga na kidato cha tano kutokata tamaa na badala yake kutakiwa kujiunga na chuo hicho kwa mpango maalumu wa kujiendeleza katika kozi mbalimbali.

Afisa Udahili wa Chuo hicho Misu Chibona amesema hayo leo katika  Maonesho ya Elimu ya Sayansi na mafunzo ya ufundi stadi (TVET) yanayoendelea Jijini hapa yenye lengo la kuhasisha wanafunzi kujiunga na vyuo vya ufundi vya kati na kueleza kuwa mpango huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaandaa wanafunzi hao katika malengo ya maendeleo endelevu na kuachana na utegemezi.

Amesema,kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi kuwavunja moyo watoto wao pale wanapo ona wameshindwa mitihani na hawawezi kuendelea na masomo kutokana na alama zao kuwa ndogo na kueleza kuwa Kila tatizo linapotokea wazizi na walezi hawapaswi kuwavunja moyo bali wanapaswa kutafuta mbinu mbadala za kukabiliana na tatizo lililopo.

Pamoja na hayo amewataka wazazi wenye watoto wanaomaliza kidato cha nne kuacha kuwakatisha tamaa wanapohitimu na kupata alama zisizoruhusu kuingia kidato cha tano bali wawapeleke chuoni hapo kujiunga na kozi zinazoendana na alama zao.

Amefafanua kuwa kutokana na kuona matukio mengi mabaya  yanayofanywa na watoto waliokatishwa tamaa na alama zao za mitihani LGTI kimeona kuna haja ya kutembelea mashuleni kuhamasisha wanafunzi kutojisikia vibaya wanapopata alama hizo bali waangalie njia nyingine ya kujiendeleza .

"Kwa kuanza tayari tumetembelea Shule zote za Sekondari katika Jiji la Dodoma na kueleza kozi tunazotoa lakini pia tuliwaambia sisi tunapokea hata mwanafunzi aliyefaulu kwa alama angalau D nne ili kusoma ngazi ya  cheti na kisha kuendelea na ngazi nyingine,"alisema  Chibona. 

Kwa upande wake Mhadhiri mwandamizi wa chuo hicho Bundala Dodo ametumia nafasi hiyo kutaja kozi zinazoruhusu mwanafunzi aliyefaulu kwa alama ya D nne kuwa ni utawala katika Serikali za Mitaa,Uhasibu na fedha,Maendeleo ya jamii,Kumbukumbu na nyaraka,Rasilimali watu na manunuzi.

Amesema,"tunataka kuokoa jamii na mwelekeo wake hususani wanafunzi wa sekondari walioshindwa kupata alama za kujiunga na elimu ya juu wasijione wakosefu wanapopata alama zisizoruhusu kuingia kidato cha tano Chuo chetu tuna kozi za kuwapeleka juu,"amesema 

Ameongeza kuwa baadhi ya wazazi wamekua mstari wa mbele kuwarudisha nyuma watoto katika kipengele cha elimu kwa kuwakatisha tamaa kwamba wakisoma ngazi ya cheti elimu yao itakuwa ndogo kitendo ambacho siyo kweli kwani mwanafunzi wao akimaliza ngazi ya cheti anauwezo wa kuendelea kupata Diploma na kuendelea zaidi hadi degree.

"Nawasisitiza wazazi mtoto akishindwa kuchaguliwa mpeleke akapate elimu inayoendana na alama zake kwasababu anayoendelea ndivyo elimu yake inavyokuwa,niwaambie wanafunzi ukisoma chuo chetu kinafaida kwasababu Serikali imetoa nafasi za ajira katika mikoa mbalimbali za watendaji wa vijiji na kata hivyo wanafunzi wakihitimu ajira zipo,"amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

1/Post a Comment/Comments

  1. Nahitaji kusoma online naweza kupata mwongozo? Na VIP kuhusu ada zenu?

    ReplyDelete

Post a Comment