BRELA YAFANYA USAFI SOKO LA MBAGALA ZAKHEIM


Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wakifanya usafi katika Soko jipya la Mbagala Zakheim lilipo katika wilayani Temeke Jijini Dar es Salaam leo Juni 20,2022 ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza rasmi Juni 16 hadi 23,2022. PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO.

Na: Hughes Dugilo, Dar es salaam


Katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma Wakala wa Usajili wa Makampuni na Majina ya Biashara (BRELA) imetoa wito kwa wafanyabiashara kote nchini kurasimisha biashara zao ikiwemo kufanya usajili ili kufanya shughuli zao na kutambulika kisheria.

Wito huo umetolewa leo Juni 20,2022 na Ofisa Habari wa Wakala huo Bi. Christina Njovu katika soko Jipya la Mbagala Zakheim walipokuwa wakifanya usafi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo yaliyoanza rasmi Juni 16 na yanatarajia kufikia tamati Juni 23, mwaka huu.

Ameeleza kuwa licha ya BRELA kufanya usafi sokoni hapo pia inawapa fursa wafanyabiashara hao kupata elimu juu ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo ikiwemo usajili wa Biashara na Leseni.

"Leo tumefika hapa kufanya usafi katika soko hili, huu ni muendelezo wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza wiki iliyopita hivyo BRELA tumekuwa tukifanya kazi mbalimbali za kijamii na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kazi zetu",amesema.

"Hii ni fursa kwa wafanyabiashara wa soko hili la Zakheim kuifahamu BRELA na kazi zake ili sasa wapate kurasimisha kazi zao kwa kusajili biashara zao,"amesema Njovu.

Ameongeza kuwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma BRELA imeendelea kutoa huduma zake za papo kwa hapo katika viwanja vya Ofisi zake zilizopo katika makutano ya mtaa wa Shaban Robert na barabara ya Sokoine Jijini Dar es Salaam na kwamba zoezi hilo litakamilika Juni 23,mwaka 2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments