TAASISI YA WOMEN ROUND TABLE TANZANIA 'MWANAMKE KINARA' YAKABIDHI MAGODORO KWA WATOTO WENYE UHITAJI MAALUM SHULE YA MBUGANI


Taasisi ya Women Roundtable Tanzania ambao ni waandaaji wa Tuzo za Mwanamke Kinara Kanda ya Ziwa imekabidhi msaada wa magodoro 80 yenye thamani ya 4,800,000 kwa watoto wenye uhitaji maalum wanaosoma katika Shule ya Msingi Mbugani iliyopo mkoani Geita.


"Tulikuja kwa ajili kukamilisha ahadi yetu tuliyoitoa mwezi wa nne kwa ajili ya watoto hawa, kwa kuzingatia huu ni mwezi maalum wa Mtoto wa Afrika hivyo watoto wote wana haki ya kupata elimu iliyo bora. Tunafanya hili kuunga juhudi za Mhe. Rais wa Awamu ya Sita na Serikali yake katika kuwapa watoto wote wa Tanzania elimu bora", amesema Khadija Liganga ambaye ni Mratibu wa Tuzo za Mwanamke Kinara.


Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbugani, Edwicka Ndunguru ameishukuru taasisi ya Women Roundtable Tanzania na wadau wake wote wakiwemo GEWOMA kwa kuwezesha upatikanaji wa magodoro hayo 80.


"Shule yetu ina changamoto nyingi lakini tunawashukuru kwa hili, tumejengewa bweni na Serikali kwa ajili ya kulala watoto 80 wenye uhitaji maalum, Shule inalea watoto 156 kukiwa na watoto wenye usonji, viziwi, wasioona, ualbino na viungo na wote wanatoka katika mazingira magumu katika familia zao", amesema Mwl. Ndunguru.


Itakumbukwa Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka tarehe 16 Juni lengo likiwa ni kuhimiza jamii kuwapa elimu kwa usawa watoto wote.

Mratibu wa Tuzo za Mwanamke Kinara Kanda ya Ziwa, Khadija Liganga (kushoto) akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magodoro hayo.
Mratibu wa Tuzo za Mwanamke Kinara Kanda ya Ziwa, Khadija Liganga na wadau alioambatana nao akikabidhi magodoro kwa uongozi wa Shule ya Msingi Mbugani mkoani Geita kwa ajili ya watoto wanaotoka mazingira magumu.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments