BABU WA MIAKA 62 ATUPWA JELA KWA KUUA MFANYABIASHARA WA MADINI MWANZA



MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza imemhukumu, Damian Andrea (62), kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kumpiga risasi na kumuua mfanyabiashara wa madini, Samwel Songoma.


Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji wa mahakama hiyo, Lilian Itemba, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo shaka.


Jaji Itemba alisema mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia ya kikatili.


Aidha, Jaji Itemba alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Janeth Kisibo, alipeleka mahakamani mashahidi tisa na vielelezo 10 ambavyo vilithibitisha kuwa mshtakiwa huyo alimuua Songoma kwa kumpiga risasi tumboni na kufariki.

Jaji Itemba alisema shahidi wa nne ambaye ni mke wa marehemu siku ya tukio alikuwa amelala na mume wake, usiku majambazi walifika na kuvunja mlango na kuingia ndani na kuamuru mumewe (Samweli Songoma) kutoa fedha.

Alisema Songoma alitoa fedha ambazo shahidi huyo hakujua ni kiasi gani, baada ya majambazi hao kupewa fedha walizunguka nyuma ya nyumba na kubomoa dirisha likaanguka juu ya kitanda.

Alisema Songoma alienda kujificha kwenye kona ya nyumba na shahidi ambaye ni mke wake alijificha chini ya kitanda.


Alisema majambazi hao walimulika tochi na kumuoma Songoma akiwa amejificha kwenye kona ya nyumba hiyo kwa ndani.

Jaji Itemba alisema majambazi baada ya kumuona Samweli kwenye kona walimlazimisha kuongeza fedha zingine, hata hivyo aliwajibu kuwa hana.


Baada ya kupewa jibu hilo, majambazi hao walimpiga risasi ya tumboni na kufariki hapo hapo.

Aidha, Jaji Itemba alisema majambazi watatu waliingia ndani na kuanza kupekua vitu ndani ya chumba hicho wakitafuta fedha.

Damian Andrea (62) ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Alisema wakati wakiendelea kupekua mke wa marehemu alimtambua jambazi mmoja kwa jina la Damiani Andrea kwa sababu alikuwa amekatika mkono wa kushoto, pia alikuwa ni fundi ujenzi katika Kijiji cha Lyobaika, Wilaya ya Bukombe.


Alisema baada ya majambazi hao kumaliza kupekuwa waliondoka na kutokomea kusikojulikana ndipo mke wa marehemu alipata nafasi ya kupiga kelele kuomba msaada wa majirani.

Jaji alisema marehemu alipelekwa Hospitali ya Geita na daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili alidai kuwa kifo cha marehemu kilitokana na damu kuvilia ndani ya tumbo kutokana na kupigwa risasi chini ya kitovu na kupasua mishipa ya damu.


Alisema Songoma alikuwa akifanya biashara ya kuuza dhahabu katika Kijiji cha Lyobaika Wilaya ya Bukombe mkoa wa Geita.


Baada ya kutoa adhabu hiyo, Jaji Itemba aliagiza bunduki moja, risasi 72 na magazine tatu vyote kwa pamoja vitaifishwe na vipelekwe serikalini baada ya muda wa rufani kumalizika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments