ALIYEKUWA MKURUGENZI WA JIJI LA ARUSHA NA WENZAKE WAFIKISHWA MAKAHAMANI KWA UHUJUMU UCHUMI



Dk John Pima aliwahi kuwa Mkururgenzi wa Jiji la Arusha kabla ya Kutumbuliwa
 ****
MKURUGENZI wa zamani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na makosa nane katika kesi mbili za uhujumu uchumi.

Pima na wenzake watatu Innocent Maduhu (aliyekuwa mchumi wa Jiji), Nuru Ginana (mchumi), Alex Daniel (mchumi), wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Bittony Mwakisu na kusomewa mashitaka nane kwenye kesi mbili tofauti za uhujumu uchumi.

Mbali na washitakiwa hao wanne, mshitakiwa mwingine ni Mariam Mshana ambaye alikuwa Mwekahazina wa Jiji hilo ambaye hakuwepo mahakamani hapo, ambapo upande wa Jamhuri umeiomba mahakama kutoa hati ya wito na kukamatwa kwa mshitakiwa huyo ambaye ni wa pili katika kesi zote.

Jamhuri imewakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Akisa Mhando na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Hamidu Simbano huku Dk Pima na Maduhu wakiwakilishwa na Wakili Valentine Nyalu.

Katika kesi ya kwanza inayowakabili Dk Pima, Mariam, Maduhu na Ginana wanakabiliwa na mashtaka manne ambayo ni ufujaji na ubadhirifu huku makosa mengine yakiwa ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.


Aidha washitakiwa hao wataendelea kukaa mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ambapo kila mmoja anapaswa kuwa na wadhamini wawili watakaoweka Sh32 milioni au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo, hadi watakapokamilisha masharti hayo.

Awali, Wakili Mhando aliwasilisha hati ya Mahakama hiyo kupewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Mei 24 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwasimamisha kazi maafisa sita wa Jiji hilo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za jiji na tuhuma za kughushi nyaraka.

Watendaji hao walisimamishwa kufuatia tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo katika kikao cha watumishi wa jiji kilichokuwa kinaongozwa na Waziri Mkuu Majaliwa.

Kufuatia tuhuma hizo zilizotolewa na mbunge huyo, Waziri Mkuu aliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru kufuatilia suala hilo.

Kesi hizo zimeahirishwa hadi Julai Mosi mwaka huu ambapo watuhumiwa hao watasomewa maelezo ya awali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments