CCU KUTUMIA BILIONI 9.6 KUNUNUA PAMBA CHATO
Na Daniel Limbe, Chato

MSIMU wa ununuzi wa pamba ukiwa umezinduliwa hivi karibuni nchini, Chama kikuu cha ushirika cha Chato (CCU) kinatarajia kutumia takribani shilingi 9.6 bilioni, kununua pamba safi kwa msimu wa 2022/23.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Greon Chandika, amesema hayo leo wakati akizungumza na mwandishi wetu aliyetaka kujua mpango mkakati ya Chama hicho kikuu cha ushirika kuhimili ushindani wa soko huria dhidi ya makampuni binafsi.

"Tayari tumeshafanikiwa kupata pesa kiasi cha shilingi 9.6 bilioni  kwaajili ya kununua pamba mbegu kutoka kwa wakulima...nimatarajio yetu kuwa tutakabiliana vizuri na ushindani wa wanunuzi binafsi".

"Kesho tunataraji kuanza kununua pamba safi iwapo taratibu za serikali zitakuwa zimekamilika ikiwemo ukaguzi wa mizani ya kupimia"amesema Chandika.

Hata hivyo,amedai kuwa Chama hicho kikuu kinao wakulima wa pamba ambao ni wanachama toka Amcos 53 zinazounda ushirika huo kwenye wilaya ya Chato na Biharamulo mkoani Kagera.

Mmoja wa wakulima wa pamba wilayani hapa mkoani Geita, Malima Mgonya, amekiomba chama hicho kikuu cha ushirika,kununua pamba kwa bei ya shilingi 2,000 kwa kila kg 1 ili kuwahamasisha wakulima wengine kuzalisha zaidi.

"Pamoja na ushindani wa makampuni ya watu binafsi tunawaomba CCU wapandishe bei ya kununulia pamba ifike angalau 2,000 kwa kila kilo moja...bei hiyo itawahamasisha wakulima wengi kurudi kwenye kilimo cha pamba ambacho wengi walikuwa wameshakitelekeza na kuhamia mazao mengine kutokana na bei kuwa chini"amedai Mgonya.

Hivi karibuni serikali ilizindua msimu mpya wa ununuzi wa pamba mbegu kwa mwaka 2022/23 huku ikitangaza bei elekezi ya shilingi 1,560 kuwa ndiyo bei ya kuanzia ikilinganishwa na msimu wa 2021/22 ambapo bei dira ilikuwa 1,050.

                 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments