CCM YAFUNGUA MILANGO MCHAKATO WA KATIBA MPYA TANZANIA..SAMIA AONGOZA KIKAO NEC

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Samia Suluhu Hassan akiendesha Kikao Cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kilichofanyika katika Ukumbi wa Jengo la Makao Makuu ya CCM la White House Jijini Dodoma, leo. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa,itikadi na Uenezi (NEC)Shaka Hamdu Shaka akizungumza na waandishi wa habari leo

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog DODOMA

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameongoza Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana leo Juni 22, 2022 katika Ukumbi wa (White House) Makao Mkuu ya CCM Jijini Dodoma ikiwa ni utaratibu wa vikao vyake vya Kitaifa.


Hatua hii imekuja baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukutana jana tarehe 21/06/2022 Ikulu Chamwino, Dodoma kwa kikao cha siku moja cha kawaida na kufuatia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanya uchaguzi wa kujaza nafasi mbili za wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa zilizokuwa wazi kwa kuwachagua kwa kura Stephen Masatu Wassira na Ndugu Theresia Adriano Mtewele.


Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa,itikadi na Uenezi (NEC) Shaka Hamdu Shaka vikao hivyo vyote viwili vimejadili masuala mbalimbali ya msingi na kwamba pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefanya uteuzi wa wenyeviti wa halmashauri za wilaya na Mameya.

Akiongea na Waandishi wa habari Jijini Dodoma leo Juni 22, 2022 Shaka amesema uteuzi huo ni Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Mji-Erasto B. Mpete ,Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
 -Mohamed Festo Bayo na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi- Stuart Nathaniel Nkinda, Apaikunda Ayo Naburi na Zuberi Abdallah Kidumo.


"Pamoja na mambo mengi yaliyozungumzwa Halmashauri Kuu ya Taifa imefanya uchaguzi wa kujaza nafasi mbili za wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa zilizokuwa wazi kwa kuwachagua kwa kura Ndugu Stephen Masatu Wassira na Ndugu Theresia Adriano Mtewele,"amesema Shaka.


MARIDHIANO NA PONGEZI KWA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN


Pamoja na mambo mengine,Katibu huyo wa itikadi na uenezi amesema kuwa miongoni mwa mambo ambayo Halmashauri Kuu imeshauri kutazamwa ni pamoja na kesi zenye sura ya kisiasa kwa wafuasi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa nchini.


Amesema Chama kimeishauri serikali utekelezaji wa masuala yote ya kuimarisha demokrasia nchini na kutaka mazingira ya kisiasa yafanyike bila kuathiri uhuru na usalama wa nchi yetu.


Licha ya hayo ameeleza kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ukomavu, ustahimilivu, uhodari na dhamira yake njema ya kufanya maridhiano na vyama vya siasa nchini kwa lengo la kuimarisha umoja, ushirikiano, mshikamano, amani na utulivu kwa maendeleo na ustawi wa watanzania wote.


"Halmashauri kuu ya Taifa imevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kukubali kuunga mkono hatua hiyo, Chama kimeishauri serikali kuharakisha utekelezaji wa masuala yote yatakayojenga kuaminiana, kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa kwa ustawi wa wananchi wote,"amesema.


Vilevile Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Husein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuonesha uvumilivu na ukomavu wa kiuongozi katika kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa hali inayochochea umoja, amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo kuharakisha maendeleo yao.


SUALA LA UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA
Kuhusu upatikanaji wa katiba mpya Shaka amesema Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kauli moja imekubaliana kuwa upatikanaji wa Katiba Mpya na kwamba Chama hicho kinakubaliana na umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na hivyo kuishauri serikali kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kwa maslahi mapana ya Taifa na Maendeleo ya watanzania wote.


Akizungumzia masuala ya uchaguzi Mkuu wa ndani ya chama,Shaka amesema Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea na kuridhishwa taarifa ya maendeleo ya uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama ambao umeshakamilika kwa asilimia 99.5 katika ngazi ya mashina na matawi kote nchini na sasa upo katika ngazi ya Kata/Wadi.


"Chama kimetakiwa kuzifanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika ngazi hizi ili kuimarisha ushiriki wa haki, usawa na demokrasia katika ngazi zote zinazofuata kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi ya Chama,"amesema
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Samia Suluhu Hassan akiendesha Kikao Cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, huku Wajumbe wakimsikiliza kwa makini, Katika Ukumbi wa Jengo la Makao Makuu ya CCM la White House Jijini Dodoma, leo. Kulia kwa Mwenyekiti, Rais Samia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana na kulia kwake ni Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo. Picha na CCM blog
Wajumbe wakiwa wamesheni ukumbi wakati wa Kikao hicho.
Wajumbe wakiwa ukumbini kwenye Kikao hicho. Kutoka kulia ni Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mmwinyi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah na Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson.
Wajumbe wakiwa ukumbini
Wajumbe wakiwa ukumbini
Wajumbe wakiwa ukumbini


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post