TUME YA UTANGAZAJI ZANZIBAR YARUDISHA HEWANI REDIO NA TELEVISHENI ZILIZOFUNGIWA…. JAZIRA CABLE TV YAFUTIWA LESENI RASMI


Mrajisi wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Sheikha Haji Daudi 
Mrajisi wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Sheikha Haji Daudi 

Na Rahma Idrisa Haji - Zanzibar

Tume ya Utangazaji Zanzibar  imerudisha hewani baadhi ya vituo vya redio na televisheni vilivyofungiwa huku  kimoja kikifutiwa leseni rasmi.

Mnamo tarehe 5/5/2022 Tume ya Utangazaji Zanzibar ilisitisha leseni za utangazaji kwa baadhi ya vituo vya utangazaji vya Redio na Television kwa kukiuka masharti ya leseni za utangazaji.

 Vituo ambavyo vilisitishwa kurusha matangazo ni BOMBA FM REDIO ,ASSALAM FM REDIO,COCONUT DIGITAL TV,AM 24 pamoja na JAZZERA CABLE TV .

Akitoa taarifa kwa  vyombo mbali mbali vya habari Mrajisi wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Sheikha Haji Daudi  ofisini kwake Kilimani Mkoa wa mjini Magharib amefafanua  kuwa kituo cha BOMBA FM Radio kilivunja masharti ya leseni kwa kurusha masafa 87.5 kinyume na masharti ya leseni iliyopatiwa katika kuomba barua ya kuwa na studio ndogo Dar es Salam yenye kumbukumbu namba TUZ /BFMR.5/VOL.1/68.

Amesema Tume ya Utangazaji Zanzibar katika kikao chake cha dharura kilichofanyika  tarehe 14/5/2022 na mambo mengine imepitia hoja za kupunguziwa adhabu kwa vituo hivyo vilivyochukuliwa hatua kutokana na kuvunja masharti ya leseni zao.


"Kwa mujibu wa kifungu cha 16( 3 )(e)cha sheria ya tume ya utangazaji Zanzibar , sheria namba 7 ya mwaka 1997 , Tume ya utangazaji Zanzibar iliamua kusitisha leseni ya kituo hicho kwa muda wa miezi sita kuanzia tarehe 5/5/2022 hadi 5/11/2022.

"Aidha tume ilikitaka kituo kuacha kabisa kurusha matangazo eneo la Unguja na Dar es Salam kwa masafa ya 87.5 MHz", amesema

Amesema  kuwa baada ya kituo hicho kuiomba Tume ipunguziwe adhabu Tume imeamua kukipa ruhusa kituo hicho kuendelea na matangazo baada ya kulipa faini iliyoelekezwa .

Kuhusu kituo cha ASSALAMU FM REDIO Mrajisi wa Tume amesema kuwa kituo hicho kilivunja masharti ya leseni kwa kubadili muundo wa hisa za kampuni bila ya kuridhiwa na kuthibitishwa na Tume ya utangazaji Zanzibar jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 44 na 58 ( 2 ) cha kanuni za utoaji leseni za utangazaji Zanzibar .

"Kutokana na kosa hilo tume iliamua kusitisha leseni ya utangazaji ya kituo hicho kwa muda wa miezi sita kuazia tarehe 5/5/2022 hadi 5/11/2022.Sambamba na kuacha kituo hicho kurusha matangazo yake eneo la Unguja na Dar es salam kwa masafa ya 92.1", amesema.

Hata hivyo Mara baada ya kituo hicho kuiomba tume kupunguziwa adhabu hiyo tume imeamua kukiruhusu kwa sasa kituo hicho kuendelea kurusha matangazo yake kwa upande wa Unguja na Dar es salam .

Akizungumzia kituo cha AM24 FM REDIO amesema kuwa kituo hicho kimevunja masharti ya leseni kwa kubadili muundo wa hisa za kampuni bila ya kuridhiwa na kuthibitishwa na tume ya utangazaji Zanzibar kinyume na kifungu cha 44 ( 1 ) na 44 ( 2 ) cha kanuni za utoaji leseni za utangazaji za mwaka 2022.


Tume ilisitisha leseni ya kituo hicho kwa muda wa miezi sita 5/5/2022 hadi 5/11/2022 na kukitaka kituo hicho kuacha kurusha matangazo yake eneo la Unguja na Dar es salam kwa kutumia masafa ya 98.5 MHz ambayo imepatiwa na Tume hiyo.

"Kituo hicho mara baada ya kuiomba tume ipunguziwe adhabu tume Imeamua kituo kipewe muda wa kurekebisha makosa yake na baada ya tume kujiridhisha basi kituo kitaruhusiwa kuendelea kurusha matangazo yake",amesema.

"Ni lazima kufanya Marekebisho haya ndipo Kituo kiendelee na Urushaji wa matangazo Ikiwemo Kuhamisha studio kuu kutoka Dar es Salam kuja Zanzibar , Kubadilisha muundo wa hisa kuendana na masharti ya kanuni za utoaji leseni za utangazaji ikiwemo kuhakikisha 51% ya hisa inamilikiwa na Mzanzibar , hata hivyo Kuwasilisha muundo mpya wa utaratibu wa urushaji wa vipindi,  hivyo kwa sasa kituo cha AM 24 REDIO Kitaendelea kutumikia adhabu yake", amesema.


Kituo cha COCONUT DIGITAL TV Tume iliamua kusitisha leseni ya utangazaji ya kituo hicho kuanzia tarehe 5/5/2022 hadi pale itakapo jiridhisha kuwa kituo hicho kipo tayari kulipa deni la USD 18,582 .

"Baada ya kituo hicho kuiomba tume kupunguziwa adhabu hiyo tume imeamua yafuatayo ; Kituo hicho kiruhusiwe kurusha matangazo kuanzia Jumamosi ya tarehe 14/5/2022 kwa kuwa kituo kimelipa USD 10,000 kwa hatua ya deni lake la mwanzo , hata hivyo kituo kinatakiwa kikamilishe malipo yaliobaki kabla ya tarehe 1 Julai 2022" amesema.

Katika hatua nyingine Tume ya utangazaji Zanzibar kwa mamlaka ya kisheria iliyopewa chini ya kifungu cha 16 ( e ) cha sheria ya tume ya utangazaji nambari 7 ya 1997 , imefuta rasmi leseni ya kituo cha JAZIRA CABLE TV kwa kushindwa kufuata maagizo ya Tume ya Utangazaji Zanzibar ikiwa ni pamoja ya kutolipa deni la Tume la USD 6000 kwa kipindi cha muda mrefu .

Sambamba na hayo  Tume ya Utangazaji Zanzibar imeviasa vyombo vya Utangazaji vinavyofanya kazi Zanzibar kufuata sheria , kanuni na miongozo pamoja na maelekezo wanayopatiwa na Tume ya Utangazaji kwa kuzingatia maadili ya habari na kutunza mila silka na tamaduni za Wazanzibar.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments