RC CHARLES MBUGE : TUCHAPE KAZI KWA BIDII UMAHIRI NA WELEDI KWA KASI INAYOHITAJIKA


Mkuu wa Mkoa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza kwenye maadhimisho ya Mei Mosi
Wafanyakazi mbalimbali waliohudhulia maadhimisho ya mei mosi
Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge na wapili mkono wa kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge akimkabidhi cheti mfanyakazi bora

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika ki Mkoa, wilayani Muleba katika Ukumbi wa Suzana Hotel, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amewahimiza wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa viwango, weledi na umahiri.


Akizungumza katika maadhimisho hayo Meja Jenerali Charles Mbuge amesema kuwa wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii, umahiri na weledi kwa kasi inayohitajika ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi tunaowatumikia.


"Sisi ni wateule ambao tumebahatika kuteuliwa kufanya kazi za wa Tanzania wenzetu, tuzingatie muda wa kazi na kutimiza majukumu ya mwajiri wetu, si vema kuwahii kutoka kazini. Tukifanya hivyo tutakuwa tumetimiza wajibu wetu na kuiachia Serikali yetu sikivu ili iweze kutufikilra katika maslahi na changamoto zilizopo katika maeneo yetu ya kazi," amesema Meja Jeneral Charles Mbuge.


Aidha, ameeleza kuwa miongoni mwa mambo yaliyofanywa na Serikali katika kuboresha maslahi ya watumishi ni pamoja na kutunga sera mpya za malipo ya mishahara na motisha kwa watumishi wa umma ikiwa ni kuundwa kwa bodi ya mishahara katika utumishi wa umma.


Lakini pia ameeleza kuwa wafanyakazi tayari Serikali imeshatoa maelekezo kwa mifuko yote ya jamii kuhakikisha wafanyakazi wanapofikia muda wa kustaafu wanalipwa mafao yao kwa wakati.


Sambamba na hayo ametoa msisitizo kwa wafanyakazi wote kuhakikisha wanatimiza wajibu wao na kuwaeleza kuwa haki inakwenda sambamba na wajibu hivyo kila mtu anatakiwa kuhakikisha  anatimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na kuondoa ubinafsi ambao ni sumu kubwa kwa wafanyakazi.


Akizungumzia Mabaraza ya wafanyakazi amewaagiza waajiri wote wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha Mabaraza yote yanakuwa hai ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria pamoja na kukutana mara mbili kwa mwaka ili kuzungumza masuala yanayowahusu watumishi.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila ametoa rai kwa wafanyakazi waliopewa tuzo za utendaji kazi bora kuendelea kutimiza majukumu mbalimbali ya waajiri wao wanapokuwa kazini na kudumisha nidhamu na uchapakazi mzuri wa kazi ili kuongeza ufanisi kwenye maeneo yao ya kazi.


Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Constansia Buhiye, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Kamati ya Usalama,  viongozi wa vyama vya wafanyakazi na watumishi kutoka sekta mbalimbali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments