ASKOFU MKONGO MAARUFU 'MZEE WA YESU' AFUKUZWA TANZANIA
Na Fadhili Abdallah,Kigoma

IDARA ya uhamiaji imemfukuza nchini Askofu Mkuu wa kanisa la House of Prayers Mukombo Muyondi Maarufu Mzee wa Yesu Raia wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kwa kuishi nchini bila vibali vya kuingia nchini wala vibali vya kazi.


Msemaji wa Idara ya uhamiaji Paul Mselle alisema hayo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mkoani Kigoma ambapo alisema kuwa kiongozi huyo amefukuzwa nchini kwa kujishughulisha na masuala ya dini bila kuwa na kibali cha kuendesha kanisa.


Kutolewa kwa taarifa hii kunafuatia kutoonekana kwa kiongozi huyo kanisani kwake kwa zaidi ya wiki moja sasa ambapo waumini wa kanisa hilo walianza maandamano ya amani kutaka kiongozi huyo kurudishwa sambamba na kutumia mitandao ya kijamii kupiga kelele kutaka kiongozi huyo alirudishwe.


Akieleza kuchukulia kwa hatua hiyo Msemaji huyo wa idara ya uhamiaji nchini alisema kuwa hii ni mara tatu kwa Askofu huyo kufukuzwa nchini ambapo mara ya kwanza alirudishwa nchini kwao Februari 2011.


“Askofu Muyondi alipewa notisi ya zuio la kuingia nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2011,pamoja na zuio hilo alipuuza na kuingia nchini kinyemela ambapo kwa kushirikiana na Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo alipewa notisi nyingine na kurudishwa nchini,”alisema Msemaji huyo.


Mselle alisema kuwa hata hivyo katika hali ya kustaajabisha askofu Muyondi ambaye pia anafahamika kwa majina ya Mulilege Mkombi Muyondi kameka alirudi tena nchini na idara ya uhamiaji kwa mara ya tatu kwa kushirikiana na Ubalozi wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo imetangaza kumfukuza na kumrejesha nchini kwao kwa mara ya tatu.


Mtuhumiwa huyo amekuwa akiendesha kanisa linalojulikana kama House of Prayers lenye makao yake makuu jimbo la Katanga Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kufungua tawi la kanisa hilo Boko Magengeni Jijini Dar es Salaam.


Hata hivyo Mtuhumiwa huyo hakutaka kuzungumza chochote mbele ya waandishi wa habari na badala yake kuwataka waandishi kufuatilia taarifa zake kwenye mitandao ya kijamii ya Instragram, facebook na twitter ambako anafahamika kwa jina la mzee wa yesu akieleza kufahamika dunia nzima.

Mchana Askofu huyo alipelekwa ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Mjini Kigoma na baadaye kupelekwa bandari ya Kigoma kwa ajili ya kurudishwa kwao

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments