Kulia ni Kamishina wa Polisi jamii Tanzania Mussa Ally Mussa akiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzora
**
Na Mbuke Shilagi Kagera.
Viongozi wa Serikali za Mitaa na Kata katika Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera wametakiwa kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao ili kupunguza vitendo vya uharifu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishina wa Polisi jamii Tanzania, Mussa Ally Mussa Mei 9,2022 alipokutana na kufanya mazungumzo na wenyeviti wa mitaa pamoja na watendaji wa mitaa na kata kwenye uwanja wa Kaitaba wilayani Bukoba mkoani Kagera ili kutoa elimu kwa viongozi hao jinsi ya kukabiliana na vitendo vya uharifu katika mitaa yao.
“Unatakiwa kujua kila nyumba wanakaa watu gani na wanashugulika na nini, ndicho kinachotakiwa ili kujua eneo lako wezi ni watu gani, hauwezi kuzuia uharifu usipo jua wahusika ni watu gani na ndo maana kazi ya Polisi inakuwa ngumu kwa sababu mnaacha vipengele vidogo, hivyo fatilieni kujua kaya za maeneo yenu wanakaa watu gani” Amesema.
Kamishina Mussa amesema kwa taarifa alizopewa na RPC wa mkoa wa Kagera vitendo vilivyokithiri katika mkoa huo kwa sasa ni mauwaji pamoja na ubakaji, na kwa taarifa alizonazo ni kwamba kipindi cha miezi mitatu inaonyesha si chini ya makosa 30 ya mauaji yanayo tokea mkoani humo.
“Bado kuna tatizo katika serikali za mitaa, hawajatambua kuwa kudumisha ulinzi katika maeneo yao ni wajibu wao kisheria wala sio ombi, wanatakiwa kujua kuwa kazi ya kulinda wananchi ni kazi yao pia siyo jeshi la polisi peke yake” Amesema.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Hamugembe iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Renovatus Mwesiga amemshukuru Kamishina wa Polisi Jamii Tanzania pamoja na viongozi wa ulinzi na usalama katika mkoa huo kwa elimu waliowapatia , huku akimuomba RPC wa Mkoa wa Kagera kuwakutanisha na polisi kata ili kuwajengea uelewa kwa pamoja.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Prof. Faustine Kamuzora amesema kuwa, wao kama viongozi katika Mkoa huo wamekuwa wakiwasisitiza sana juu ya umuhimu wa kudumisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali ya mkoa licha ya mkoa huo kuwa na idadi kubwa ya watu huku ameahidi kuendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha wananchi wa mkoa huo wanakaa kwa Amani na usalama.
Social Plugin