TASAF YATOA ELIMU YA USTAWI WA JAMII KWA WANUFAIKA WA TASAF HALMASHAURI YA ARUSHA


Mratibu wa TASAF Grace Makema akitoa elimu ya ustawi wa jamii kwa wanufaika wa TASAF


Na Rose Jackson,Arusha

Halmashauri ya Arusha inatekeleza mkakati wa kutoa elimu ya Ustawi wa Jamii kwa wanufaika wa mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, mradi unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wanufaika hao wa matumizi ya ruzuku ya fedha wanazopokea ili kufikia malengo ya serikali.

Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Arusha, Grace Makema, amesema kuwa, kila zoezi la ugawaji fedha linapofanyika, watalamu huhakikisha wanatoa elimu kwa walengwa juu ya mambo muhimu ya kijamii, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa namna bora ya matumizi ya fedha hizo, pamoja na kuwapa uelewa juu ya malengo ya serikali kutoa ruzuku hiyo kwa kaya zenye uhitaji.

Aidha amefafanua kuwa, serikali inatoa fedha hizo zikiwa na masharti ya kuzingatia, hivyo walengwa wa TASAF wanatakiwa kufahamu masharti ya fedha za ruzuku wanazopokea, pamoja na kuyatekeleza kwa usahihi, ikiwemo ruzuku ya msingi, ruzuku ya elimu na ruzuku ya afya kwa kaya hizo.

"Tunalazimika kutoa elimu, kutokana na uzoefu wa walengwa wanaopokea fedha kushindwa kutekeleza masharti na ruzuku na kusababisha kupoteza sifa, kama Halmashauri, tumejipanga kuwakumbusha kuzingatia masharti ya ruzuku ya fedha hizo, ikiwemo kuhakikisha watoto wanaosoma wanahudhuria masomo, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kuhudhuria kliniki, na zaidi kuhakikisha ruzuku ya msingi inatumika kupata mahitaji muhimu na kuendelza pato la familia", amesema Makema.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii, kata ya Mwandeti, Paulina Masoka, amekutwa na Kamera yetu akitoa elimu kwa Walengwa wa kijiji cha Losinoni kati, kata ya Oldonyowas, na kuweka wazi kuwa, ni kawaida kabla ya walengwa kupokea pesa, kupewa elimu ya masuala mbalimbali ya kijamii, yaliyopo na yanayoendelea kila siku.

"Hapa tunakumbushana, juu ya kuzingatia masharti ya ruzuku ya fedha wanazopoke pamoja na matumizi sahihi ya fedha hizo, zaidi tunawahamasisha kuunda vikundi vya kuweka na kukopa, lakini pia tumekumbushana juu ya malezi bora ya familia kwenye masuala ya Lishe bora na unyonyeshaji kwa watoto kwa siku 100, watoto kuhudhuria shuleni, kuwapeleka watoto kliniki, kujitokeza kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi mwezi Augost 2022, pamoja na kuwapeleka watoto kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio", amesema Paulina.

Hata hivyo wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini, kijiji cha Losinoni kati, wamewapongeza wataalam kwa kuwapa elimu itakayowafanya kutambua msingi wa ruzuku ya fedha wanazopokea pamoja na malengo ya serikali ya kuzikwamua kaya hizo kutoka kwenye hali ya uamsikini.

Mwenyekiti wa kijiji cha Losinoni kati, mheshimiwa, Peter Gabriel, licha ya kuishukuru serikali kwa kutoa ruzuku kwa kaya zenye uhitaji, ameipongeza Halmashauri kwa kutoa elimu kwa walengwa wa TASAF, kutokana na ukweli kuwa elimu hiyo itawawezesha kujikwamua kijamii na kiuchumi, hali itakayosababisha kuondokana na wimbi la umasikini uliokuwa unazikabili kaya hizo.

Mnufaika wa TASAF, Amani Ngeresa amewashukuru na kuwpaongeza watalamu, kwa kuwapa elimu inayowezesha kutambua namna ya kuzingatia masharti ya ruzuku, matumizi sahihi ya fedha hizo, elimu iliyowawezesha kufahamu lengo la serikali la kuondoa umasikini kwenye kaya zao.

"Tunashukuru kwa elimu tuliyopewa, awali hatukufahamu kuwa pesa hizo zina masharti yake, na hatukufahamu lengo la Serikali kwa undani, lakini sasa tumejua serikali inataka nini kwetu, na tunaahidi kutumia pesa hizi, kuunda vikundi vya kuweka na kukopa ili kupata mitaji ya kuanzisha biashara ndogogo ambazo tunaamini zitatuondoa kwenye umaskini uliokuwepo.",amesema Amani.

Awali halmashauri ya Arusha, ni miongoni mwa halmashauri zinazonufaika na mradi wa Mpango wa Kunusuru kaya masikini, unaotekelezwa na TASAF III, huku jumla ya kaya 13, 859 katika vijiji vyote 88 vya halmashauri ya Arusha zikinufaika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post