STAMICO NA ABSA WASAINI MKATABA WA KUUZIANA MAKAA YA MAWE


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse akibadilishana Mkataba na Rais wa Kampuni ya ABSA, Bw.Gerges Schmickrath huku Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa akishuhudia utiaji saini mkataba huo leo Mei 10,2022 jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse na Rais wa Kampuni ya ABSA, Bw.Gerges Schmickrath wakionyesha Mktaba baada ya kusaini huku Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa akishuhudia utiaji saini mkataba huo leo Mei 10,2022 jijini Dodoma.
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa akishuhudia utiaji saini mkataba mnono kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya ABSA.Kulia kwake ni Kampuni ya ABSA, Bw.Gerges Schmickrath na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse,hafla hiyo imefanyika leo Mei 10,2022 jijini Dodoma.
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa,akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba mnono kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya ABSA ya nchini Uswiss leo Mei 10, 2022 jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk Venance Mwasse,akizungumza mara baada ya kusaini Mktaba mnono na Kampuni ya ABSA ya nchini Uswiss hafla iliyofanyika leo Mei 10, 2022 jijini Dodoma.
Rais wa Kampuni ya ABSA, Bw.Gerges Schmickrath,akiishukuru wizara kupitia STAMICO kwa kuaminiwa kuwekeza katika mradi wa makaa ya mawe mara baada ya kusaini mkataba huo leo Mei 10,2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Drumlin Construction LTD ambaye ni msafirishaji wa makaa hayo nchini, Linus Seushy,akielezea jinsi alivyojiandaa kuhakikisha kila kitu kinafanyika kama kilivyopangwa kwakuwa ni jambo la kihistoria kwa nchi.
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba mnono kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya ABSA ya nchini Uswiss leo Mei 10, 2022 jijini Dodoma.

……………………………………………..

Na Alex Sonna-Dodoma

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO), na Kampuni ya Kimataifa ya ABSA inayojihusisha na masuala ya Uchimbaji wa makaa ya mawe ya nchini Uswiss wamesaini mkataba mnono wa miaka mitano wa mauziano ya tani 60,000 kwa mwezi za makaa ya mawe.

Akizungumza leo Mei 10,2022 jijini Dodoma mara baada ya kusaini mkataba huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk Venance Mwasse amesema kuwa mkataba huo ni mkubwa ni kihistoria kwa nchi kwakuwa utasaida kwenye masuala ya kiuchumi.

Dk.Mwasse amesema kuwa kupitia mkataba huo, tani za makaa ya mawe 60,000 yatazalishwa kwa mwezi ambapo kwa kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji kiasi cha sh. Bilioni 250 zitazalishwa kama mapato.

“Makaa hayo yatasafirishwa kutoka Kiwira hadi Bandari ya Mtwara na tayari magari 300 yatakayokiwa na madereva wawili kila moja yameandaliwa hivyo watakuwa 600 jumla, pia kutakuwa na nguvu kazi takribani watu 200,”.

‘Kwa kiasi kikubwa mapato yataongezeka zaidi kutokana na namna tutakavyotekeleza kupitia vifungu tulivyokubaliana kwenye mkataba, hivyo niwahakikishie ABSA kupo mpo kwenye mikono salama tunaahidi matokeo mazuri na huduma nzuri kwenu,”amesema Dk.Mwasse

Aidha Dk,Mwasse amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni matokeo ya mkakati wa kwanza wa uchimbaji makaa ya mawe ambao maandalizi yake yamekamilika na mchakato unaanza.

Kwa upande wake Rais wa Kampuni ya ABSA, Bw.Gerges Schmickrath ameishukuru wizara kupitia STAMICO kwa kuaminiwa kuwekeza katika mradi wa makaa ya mawe. Amesema, mradi huo utakuwa na manufaa kwa watanzania kwa kuongeza pato la Taifa.

“Kupitia mkataba huu nawashukuru sana nchi ya Tanzania kwa kukubali maana hili suala tumelifanyia kazi miezi miwili hadi leo tumefikia kwenye uamuzi mzuri, tunaahidi tutafanya kazi nanyi maana yakiwepo mafanikio ni yetu sote so ya upande mmoja,”.

Naye Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa STAMICO itakusanya mapato wastani wa shilingi bilioni 4.16 kwa mwezi sawa na wastani wa shilingi bilioni 50 kwa mwaka.

Pia, STAMICO itatoa ajira za zisizo za moja kwa moja 600 na fursa nyingine za ajira kwa Watanzania katika mradi huo.

Hata hivyo Dkt,Kiruswa amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt.Venance Mwasse na Menejimenti yake kwa kuwa wabunifu katika kutafuta masoko nje ya nchi. Aidha ameishukuru STAMICO kwa maamuzi ya kukubaliana na Kampuni ya ABSA katika kufanya biashara nchini.

“Ni matumaini yangu kuwa makubaliano haya yaliyosainiwa yatakuwa na manufaa kwa pande zote mbili,”amesema Dkt.Kiruswa.

Hata hivyo amesema kuwa Kama wizara wamejipanga kuhakikisha afya ya mazingira inaimarishwa vizuri wakati wa usafirishaji, pia sheria, kanuni na taratibu zilizopo zimewekwa vizuri ili kuhakikisha wawekezaji wanakua salama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Drumlin Construction LTD ambaye ni msafirishaji wa makaa hayo nchini, Linus Seushy amesema kuwa wamejiandaa kuhakikisha kila kitu kinafanyika kama kilivyopangwa kwakuwa ni jambo la kihistoria kwa nchi.

Hafla ya utiaji saini mkataba wa makaa ya mawe ya Mkoa wa Songwe katika mgodi wa Kabulo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Madini na Shirika la Madini la Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments