FUNDI : HAKUNA VITUO MAALUMU VYA KUHESABIA SENSA


Meneja wa takwimu na Mratibu wa sensa Mkoa wa Kagera Bw. Fabian Fundi akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya sensa ya watu na makazi katika Mkoa wa Kagera.
Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Mlima wa Bwana Tanzania lililopo kata ya Kashai mtaa wa Kilimahewa Mch. Francisco Felician akizungumzia zoezi la sensa ya watu na makazi.


Na Mbuke Shilagi Kagera.
Meneja wa Takwimu na Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoa wa Kagera Bw. Fabiani Fundi amesema kuwa hakuna sehemu maalumu ya kuhesabia sensa isipokuwa Karani wa sensa ataenda kwenye kaya.


Kauli hiyo ameitoa wakati alipotembelewa na mwandishi wa habari ofisini kwake ili kujua maandalizi ya sensa katika Mkoa wa Kagera na kusema kuwa maandalizi tayari yameshafanyika kwa kutenga maeneo ya kuhesabia kwa kumsaidia Karani wa sensa kutokuhesabu mtu mara mbili na kwamba hakuna vituo maalumu vya kuhesabia sensa kama ambavyo watu wamekuwa wakimuuliza.


"Kuna mtu aliniuliza kutakuwa na vituo vingapi vya kuhesabia Muleba nikamjibu hapana, sisi hatutengenezi vituo vya kuhesabia kama uchaguzi, Karani wa sensa ataenda kwenye kaya ya kila mtu", amesema.


Bw. Fundi amesema kuwa siku ya Sensa ya Watu na Makazi itakuwa tarehe 23 Agosti mwaka huu ambayo itakuwa ya siku tatu na kwamba hakuna shughuli yoyote ya kiuchumi itakayosimamishwa kwa ajili ya zoezi la sensa badala yake wale makarani watatembelea sehemu zote kuhakikisha kila mtu anahesabiwa popote atakapokuwa huku shughuli zikiendelea.


"Mtu alipo lala siku ya kuamkia sensa ndipo atakapohesabiwa pale alipo awe mtanzania asiwe mtanzania atahesabiwa, yapo maeneo maalumu yatakayohesabiwa saa sita usiku wa kuamkia sensa ambayo ni stendi, viwanja vya ndege, nyumba za wageni kwa hiyo itakapofika saa sita usiku atahesabiwa maana wale niwasafiri wataamka wameondoka hivyo watahesabiwa usiku huo, na kwenye kaya makarani wataenda asubuhi", amesema.


Aidha amewaomba wananchi kutoa taarifa sahihi ambazo zitaliwezesha Taifa pamoja na wadau wengine wa maendeleo kupanga mipango kulingana na makundi maalumu katika eneo sahihi.


"Na inawezekana Kagera kuna watu wenye walemavu wengi kuliko mikoa mingine lakini tukiwaficha tunaweza kuletewa bajeti kidogo kumbe tuna aina flani ya makundi ni wengi hivyo watu watoe taarifa sahihi na wasiwafiche watu wenye ulemavu.


"Hata ulipo toka nyumbani umefanya sensa kwamba una watu wangapi, na una watoto wangapi wanahitaji maziwa, una mama mjamzito anahitaji huduma, kwa hiyo takwimu hiyo kwenye kaya yako inakupa mwelekeo wa kutoa mahitaji, ambayo ni sawasawa na Serikali ina watoto 50 italeta bajeti ya Chanjo ya watoto 50 kumbe wewe ulificha wapo 100 usiilaumu Serikali ni takwimu uliyoitoa, nawaomba tu wananchi mtoe takwimu sahihi", amesema.


Ameongeza kuwa sensa hii ni ya sita na kwamba sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967, ya pili mwaka 1978, ya tatu mwaka 1988, ya nne mwaka 2002, ya tano mwaka 2012 na ya sita inafanyika mwaka huu na kwamba maoteo ya mkoa wa Kagera watu watakaohesabiwa ni milioni tatu.


Kwa upande wake Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Mlima wa Bwana Tanzania lililopo kata Kashai mtaa wa Kilimahewa Mch. Fransisco Felician amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani ili Serikali inapotoa bajeti itoe kiusahihi kulingana na idadi iliyopo na kwamba watu waondoe mawazo potofu wakubali kuhesabiwa.

"Sensa inapofanyika inasaidia Serikali kutoa huduma sahihi kwa watu wake, usipo hesabiwa wewe kuna matumizi makubwa utayatumia ambayo sio ya kwako kama vile Afya na Elimu, na ili zoezi liende kikamilifu ni wewe kutoa taarifa sahihi",amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments