MTUHUMIWA AWASHAMBULIA POLISI AKITUMIA NYUKI... BALAA KITUO CHA POLISI


Mshukiwa aliyeshtakiwa kwa wizi katika Kituo cha Polisi cha Kathiani, Kaunti ya Machakos nchini Kenya amewabwagia nyuki maafisa wa polisi katika jaribio la kutoroka kizuizini.

Katika ripoti ya polisi, iliripotiwa kuwa nyuki hao mara ya kwanza walimvamia afisa mmoja aliyekuwa akifungua seli ya mshukiwa mnamo Jumatano, Mei 4,2022.

Kabla ya tukio hilo mshukiwa alimtupia uchafu afisa mmoja aliyefahamika kwa jina la David Mambo aliyekuwa akimfunga pingu.


“Mshukiwa alimtupia uchafu na mara nyuki hao walianza kuwavamia askari huku mshukiwa akijaribu kutoka nje lakini askari waliwavumilia nyuki hao na kufanikiwa kumfunga pingu mshukiwa,” ripoti ya polisi ilidokeza.

Polisi hao waliongeza kuwa maafisa wengine wanne waliokuwa wamefika katika eneo la tukio ili kumuokoa mwenzao walipelekwa katika hospitali ya Kathiani Level 4 na wanauguza majeraha ya kudungwa na nyuki.

Maafisa hao wa polisi wa Machakos walidokeza kuwa wanachunguza kisa hicho ili kubaini jinsi nyuki waliingia seli zao bila wao kujua.

"Mshukiwa pia amepewa dawa na sasa yuko katika seli katika kituo cha polisi cha Kathiani akisubiri kufikishwa mahakamani," ilisoma ripoti ya polisi.

 Katika kisa tofauti, maafisa wa kituo cha polisi cha Lolgorian, Kaunti ya Narok walilazimika kutoroka kituoni baada ya kundi la nyuki kuvamia kituo hicho.

Afisa mmoja alijeruhiwa katika tukio hilo na kupelekwa katika hospitali ya kaunti hiyo akiwa na majeraha mabaya. 

“Afisa Peter Onyango alipelekwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Nyayo level 4 ambako alitibiwa na baadaye kuruhusiwa akiwa katika hali nzuri. 

"Wengine walijificha katika afisi zao na hawakushambuliwa vikali. Juhudi za kuwaondoa nyuki hao kutoka eneo la kituo zinaendelea," ilisoma ripoti ya polisi.

 Polisi hao pia walifichua kuwa walikuwa wameanzisha uchunguzi kuhusu shambulio hilo la nyuki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments