MAWAKILI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA BIDII


Katibu mkuu wizara ya katiba na sheria Mary Makonde akifungua mafunzo ya mawakili wa serikali yanayofanyika Arusha kwa siku nne

Na Rose Jackson,Arusha

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makonde amewataka mawakili kuendelea kufanya kazi kwa bidii , uadilifu na umakini katika utekelezaji wa kazi zao.


Mhe. Makonde ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya mawakili wa serikali yanayofanyika jijini Arusha.


Amesema kuwa mawakili wanapaswa kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa bidii kwenye taasisi ambazo wanafanya kazi ambazo wamekabidhiwa majukumu ya kutoa ushauri na kuhifadhi nyaraka.


Aidha amewataka mawakili hao kutumia mafunzo hayo vizuri huku akiwataka kwenda kuwa wakufunzi kwa wale ambao hawakushiriki mafunzo hayo.


Ameongeza kuwa wizara ya katiba na sheria itaendelea kuwajengea uwezo mawakili ili wafanye kazi kwa weledi na kwa kiwango cha juu.

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa ofisi ya wakili mkuu wa serikali mwaka 2018 wamepata mafanikio mengi ikiwemo kuokoa zaidi ya shilingi trilioni kumi kupitia mashauri wanayoendesha ndani na nje ya nchi..
Malata ametaja changamoto zinazowakabili ofjsi ya wakili mkuu wa serikali kuwa ni pamoja na upungufu wa watumishi kwenye maeneo mtambuka haswa kada ya mafuta na gesi pamoja na upungufu wa vifaa vya tehama na vitendea kazi .


Akizungumza kwa niaba ya mawakili wanaoshiriki mafunzo hayo Jenifa Kaaya wakili mwandamiizi wa serikali kutoka ofisi ya wakili mkuu wa serikali amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo na uelewa na anaamini watatoka hapo wakiwa na nguvu kubwa kuliko hapo awal.


Jumla ya taasisi za serikali 90 pamoja na wizara 24 zinashiriki mafunzo hayo ambayo yanalenga kuwajengea uwezo mawakili taasisi za serikali pamoja na wizara.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post