GGML YATOA MSAADA WA MAGARI MANNE VETA MWANZA


Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti Geita Gold Mining Limited anayeshughulikia miradi endelevu kwa nchi za Tanzania na Ghana, Simon Shayo (katikati) akikabidhi kadi ya gari kama ishara ya kukabidhi msaada wa magari manne ambayo GGML imeyatoa kwa Chuo cha VETA tawi la Mwanza. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala na kushoto kwake ni Kaimu Mkuu Mkurugenzi Mkuu wa Veta Kanda ya Ziwa, Charles Kaugele.
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa msaada wa magari manne aina ya Toyota Land Cruiser kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini (VETA) tawi la Mwanza.

Magari hayo ni muendelezo wa msaada wa kampuni ya GGML kwa taasisi mbalimbali nchini katika kuzisaidia kuetekeleza majukumu yake ya kila siku.


Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya magari hayo, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti Geita Gold Mining Limited anayeshughulikia miradi endelevu kwa nchi za Tanzania na Ghana, Simon Shayo amesema msaada huo umetolewa muda muafaka na unaendana na malengo endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.

“Tumeunga mkono juhudi za Veta kwasababu kwa kiasi kikubwa wanafunzi wanaotoka Veta ni wanafunzi wa kiutendaji ambao unamfanya mtu akitoka akafanye kile kitu ambacho amejifunza.


“Kwa upande wa mafunzo ya udereva na ufundi wa magari tunadhani kwamba janga kubwa lililopo ni ujuzi mdogo wa watu wanaotumia vyombo vya moto yakiwemo magari, kwa hiyo mtu akipitia mafunzo kama haya ya VETA akitoka hapo atakuwa dereva bora zaidi,” amesema na kuongeza;


“Huu ni mwendelezo wa ubia wetu na VETA wa muda mrefu ambapo tumekuwa tukifadhili mradi wa kufunza wanagenzi kwa ajili ya sekta ya madini tumefadhili karibu watu 130 kutoka kwenye jamii inayotuzunguka na wameajiriwa kwenye migodi kama mafundi wakubwa ikiwa ni mwendelezo wa kuongeza ajira kwa watanzania,” amesema.


Amesema GGML inawajibu wa kuinufaisha jamii kutokana na shughuli yake ya uchimbaji dhahabu. Mwanza ni majirani zetu na wakati tunaanza uchimbaji mwaka 2000, Geita ilikuwa mkoa wa Mwanza.


“Baada ya kuona changamoto ya usafiri kwa Mamlaka ya VETA jijini Mwanza, tumeamua kutoa msaada wa magari haya ili kuboresha mazingira ya utoleaji wa elimu kwa vijana wetu wanaosomea ufundi lakini pia kuendana na lengo la nne la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa linalosisitiza ubora wa elimu,” alisema Shayo.


Kaimu Mkuu Mkurugenzi Mkuu wa Veta Kanda ya Ziwa, Charles Kaugele ameipongeza GGML kwa msaada huo akisema utasaidia pia kutoa mafunzo kwa vitendo wanafunzi wanaosomea udereva chuoni hapo.

Tangu mwaka 2006 kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imekuwa ikishirikiana vizuri na VETA kwa kusomesha vijana 130 katika mafunzo jumuishi ya ufundi katika madini.


Idadi kubwa ya vijana hao wameajiriwa na GGML na wanatoka katika mitaa ya Geita ikiwemo Uwanja 14 Kambarage, Compound, Bugulula, Ujamaa, Mwatulole, Mission pamoja na Nyerere road.

GGML imekuwa kinara wa uwekezaji kwenye jamii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ambapo vipaumbele vikuu vimekuwa ni miradi ya elimu, afya, maji, barabara, miradi ya kukuza kipato na miradi mingine mingi ya kijamii ili kuhakikisha jamii mwenyeji inapata maisha bora.


Mapema mwaka huu, GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka wa fedha 2020/2021 baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa mapato (kodi) na uendelezaji wazawa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post