WANAHISA WA BENKI YA CRDB WAIDHINISHA MALIPO YA GAWIO LA BIL. 94 KWA MWAKA WA FEDHA WA 2021


Wanahisa wa Benki ya CRDB wamepitisha kwa kauli moja mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi kuhusu malipo ya gawio la Shilingi 36 kwa kila hisa ambayo yanaleta jumla ya thamani ya gawio la mwaka wa fedha 2021 kufikia Sh 94 bilioni.


Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 27 wa Benki hiyo uliofanyika jana katika mazingira ya mseto, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo Dkt. Ally Laay alisema gawio lililoidhinishwa kwa kila hisa ni ongezeko la asilimia 64 ikilinganishwa na Shilingi 22 kwa kila hisa iliyotolewa mwaka jana. Alisema hiyo inaashiria ukuaji wa mapato kwa kila hisa ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 yalikuwa Shilingi 102.7.
"Kwa mara nyingine tena, tunafuraha kuwasilisha thamani endelevu kwa Wanahisa wetu. Utendaji wa Benki katika mwaka wa 2021 ulitoa matokeo mazuri sana, ambayo unadhihirisha mafanikio ya mikakati yetu ya biashara. Mwaka 2021 Benki ilipata faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 268.2 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62.3,” alisema Dkt. Laay.

Aidha alibainisha kuwa kampuni tanzu za Benki hiyo ziliendelea kuchangia vyema katika biashara ya kundi huku kampuni tanzu ya Burundi pekee ikichangia faida ya jumla ya Shilingi bilioni 12.8 huku kampuni tanzu ya bima ikichangia faida ya TZS 859.0 milioni. Jumla ya mchango wa kampuni tanzu kwenye faida ya kundi ilikuwa 5%.
" Nafurahi kuripoti kwenu kwamba tumepata maendeleo makubwa katika kupata leseni na vibali vinavyohitajika kutoka kwa mamlaka za nyumbani pamoja na DRC. Tunatarajia kuanza uendeshaji ndani ya nusu ya pili ya mwaka wa fedha wa 2022.,” alibainisha alipokuwa akiwasasisha wanahisa kuhusu upanuzi wa kimkakati wa Benki hadi DRC.

Akizungumzia utendaji wa mwaka uliopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema mapato ya uendeshaji ya Kampuni yaliongezeka kwa asilimia 14.3% hadi Shilingi bilioni 924.0 kutoka Shilingi bilioni 808.7 mwaka 2020. Ukuaji huo ulitokana na ongezeko la 11.3% ya mapato ya jumla ya riba, yaliyotokana na ukuaji mzuri wa mikopo kwa wateja wadogo na wakati. Pamoja na ukuaji wa mikopo Benki hiyo lilifunga mwaka na uwiano wa mikopo chechefu wa 3.3% kulinganisha na kiwango cha udhibti cha soko cha 5%.
Nsekela alisema Benki ya CRDB pia ilirekodi ukuaji mkubwa wa mizania wa mwaka hadi mwaka wa 23% kutoka Shilingi trilioni 7.2 i mwaka 2020 hadi Shilingi trilioni 8.8. Ukuaji huo ulisababishwa na ukuaji wa asilimia 19.4 wa amana za wateja hadi Shilingi trilioni 6.5 kutoka Shilingi trilioni 5.4 zilizoripotiwa mwaka 2020, na ukuaji wa 20.6% wa fedha za wanahisa.

"Kutokana na mtazamo wetu makini katika mwaka huo, Benki yetu iliendelea kukamata masoko kwa bidhaa na huduma bunifu, hivyo kupelekea ukuaji endelevu katika mapato na faida yetu. Tuliendelea kufanyia kazi changamoto za wateja ili kuboresha utoaji wetu wa huduma na kuhakikisha tunawapa uzoefu uliobora zaidi pindi watumiapo huduma zetu,” aliongeza.
Akizungumzia kuhusu mipango ya mbeleni, Nsekela alisema kipaumbele cha Benki hiyo ni kuimarisha vichocheo vya ukuaji, na kujenga misingi imara ya uendelevu. Alitaja mwaka wa fedha wa 2022 kuwa mwaka wa mwisho wa mkakati wa muda wa kati wa Benki ya CRDB ambao ulikuwa na jukumu muhimu katika kuimarisha utendaji, na umeipa msingi mzuri benki hiyo kukabiliana na siku zijazo.

Aliwashukuru wanahisa kwa imani yao na kuendelea kuunga mkono uongozi na wafanyakazi wa benki hiyo, ambako kumeiwezesha benki hiyo kupata mafanikio makubwa katika sekta ya huduma za kifedha Tanzania, na kuwahakikishia dhamira ya Benki hiyo ya kuendelea kutoa thamani endelevu zaidi kwao.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo, Dkt. Ally Laay aliwaeleza wanahisa kwamba katika kipindi cha mwaka huo, Benki ya CRDB ilipokea Wajumbe wapya wa Bodi Bw. Gerald Kasato, aliyechukua nafasi ya Bi. Rose Metta, akiwakilisha wanahisa wanaomiliki kati ya 1% -10% ya hisa na Bw. Roya Lyanga aliyechukua nafasi ya Bi. Ellen Gervas Rwijage kama mwakilishi wa Mfuko wa Uwekezaji wa DANIDA (DIF).

Bodi pia ilimteua Bi. Jessica Nyachiro kuongoza kampuni tanzu ya Benki ya CRDB katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Hadi kuteuliwa kwake, Bi. Nyachiro alikuwa Mkuu wa Mikakati na Mahusiano ya Wawekezaji. Pia alifahamisha wanahisa Afisa Mkuu wa Biashara wa muda mrefu wa Benki hiyo Dkt. Joseph Witts alitimiza umri wake wa kustaafu Desemba 2021. Hata hivyo, Bodi ilimuongezea mkataba wa miezi sita ili kuruhusu kukamilika kwa zoezi la kuajiri.

Kwa upande mwingine, Wanahisa waliidhinisha Ernst & Young kama Wakaguzi wa Nje wa Benki kwa mwaka wa fedha wa 2022, kuashiria imani yao katika sheria ya kiakili ya kampuni na kuendelea kwa Benki kuzingatia itifaki za utawala bora.

Wanahisa wa Benki pia walimchagua tena Wajumbe watatu wa Bodi Bw. Abdul Ally Mohamed kuwakilisha wanahisa wenye umiliki chini ya 1%, Dk. Fred Msemwa kuwakilisha wanahisa wenye hisa kati ya 1% na 10%, Bw. Martin Warioba kama Mkurugenzi Huru.

Akizungumzia malipo ya gawio hilo, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Benki hiyo na Mbunge wa Vunjo, Dkt. Charles Kimei, alieleza kufurahishwa kwake na kuendelea kuongezeka kwa gawio huku akibainisha kuwa ukuaji huo ni mkubwa kupata kutokea. Dkt. Kimei alisema kuwa hisa za benki hiyo zimebakia kuwa chachu ya wawekezaji kwasababu benki hiyo haijawahi kushindwa kutoa gawio kwa Wanahisa wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post