MREMA NA MKEWE WAHITIMISHA FUNGATE LAO KIBABE

 MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Taifa, Dkt.Augustine Lyatonga Mrema ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuimarisha ulinzi kwenye hifadhi zilizopo nchini kwa kushirikiana na vikosi vya ulinzi ili kuweza kukabiliana na tatizo la ujangili.

Ametoa wito huo wakati akizungumza katika mahojiano na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake ya siku sita kwenye hifadhi nne za wanyama akiwa na mke wake Doreen Kimbi kwa ajili ya kukamilisha fungate yao.

Mrema amesema pamoja na kwamba kumeimarishwa kwa vikosi vya ulinzi kwenye hifadhi lakini bado wananchi ambao vijiji vyao vipo karibu na hifadhi wana nafasi ya kusaidia ulinzi ili kumaliza tatizo la ujangili.
Aidha, Mrema amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi za wanyama badala ya kidhani kuwa kazi hiyo ni kwa ajili ya wageni tu kutoka nje.

Amesema Watanzania wanapaswa kumuunga mkono rais Samia Suluhu Hassan ambaye amejipanga vizuri kwa ajili kutangaza vivutio vyetu vya utalii ndani na nje ya nchi kupitia filamu ya Safari Royal Tour kwa kutembelea mbuga za wanyama.
"Nimekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani y Nchi, nimekuwa Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, nimekuwa Naibu Waziri Mkuu, nimekuwa mbunge Vunjo lakini sikuwahi kutembelea kwenye mbuga za wanyama lakini kiukweli kuna mambo mazuri ya kujifunza unapopata fursa usikose kutembelea hifadhi zetu,"amesema.


Naye mke wake Mrema, Doreen Kimbi, amesema katika mbuga za wanyama kuna vitu vingi vizuri vya kujifunza hivyo wananchi kila mwezi wewe wanapanga ratiba kutembelea hifadhi zetu.
Doreen amesema wazo la kufanya fungate kwenye hifadhi za wanyama alilitoa yeye na mume wake (Mrema) kulikubali haraka kwani hiyo ndio njia mojawapo ya kumuunga mkono rais Samia ambaye amekuwa akisisitiza umuhimu wa wananchi kutembelea hifadhi zetu zilizopo nchini.

Naye Afisa Uhifadhi Utalii wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, Renard Twinzi amesema, katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Aprili 2022 hifadhi hiyo imetembelewa na watalii 57,485.

Amesema, hifadhi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa utalii imeweka mikakati ya kuhamasisha utalii wa ndani ili kuweza kufikia malengo ya hifadhi kutembelewa na 100,000 kwa mwaka.
Mrema na mke wake katika ziara hiyo iliyopewa jina la Mr&Mrs Mrema Honeymoon Tour walitembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tarangire, Manyara na Ngorongoro ambazo zimezungukwa na maliasili nyingi nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments