JINSI TANZANIA ILIVYOADHIMISHA SIKU YA USALAMA NA AFYA DUNIANI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, akihutubia wadau mbalimbali waliojitokeza katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya Usalama na Afya mahali pa kazi iliyoadhimshwa Kitaifa Mkoani Dodoma katika viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre.


Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda akizungumza na wadau mbalimbali walijitokeza katika hafla za kilele cha maadhimisho ya kimataifa ya wiki la usalama na afya mahali pa kazi mkoani Dodoma, miongoni mwa aliyozungumza ni Pamoja na namna ambavyo maadhimisho hayo yameleta fursa kwa wakazi wa Mkoa huo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako (wapili kushoto), akikabidhi tuzo kwa mwakilishi wa moja ya makampuni yaliyoshinda tuzo za Usalama na Afya mahali pa kazi na OSHA ikiwa ni miongoni mwa shughuli za maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani Aprili 22, 2022.


Mkaguzi wa Mazingira ya Kazi wa OSHA, Bw. Simon Lwaho (aliyeshika kipaza sauti) akimfafanulia, Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa katika banda la maonesho la OSHA. Huduma hizo ni usajili wa maeneo ya kazi, elimu ya usalama na afya mahali pa kazi, vipimo vya maonjwa yatokanayo na kazi.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Pro. Joyce Ndalichako (katikati), Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga (mwenye ushungi), Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.Bw. Kaspar Kaspar Mmuya Pamoja na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda (mwenye kilemba) wakitembelea mabanda ya maonesho mara baada ya hafla za madhimisho kumalizika.


Vikundi vya vya ngoma za asili vya Nyati na Nyota vikitoa burudani kwa viongozi na wadau mbalimbali waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya wiki la usalama na afya mahali pa kazi duniani katika viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre Mkoani Dodoma.


Bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT-Brass Band) Makutupora ikiongoza maandamano ya wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya kazi katika kilele cha maadhimisho ya wiki la usalama na afya mahali pa kazi duniani Aprili 28, 2022.

************************

Na Mwandishi Wetu

Aprili 28 kila mwaka ni siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambapo jana Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani katika kuadhimisha siku hiyo.

Maadhimisho hayo mwaka huu yamefanyika kitaifa jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako.

Kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu ni: Kwa Pamoja tushirikiane kujenga utamaduni bora wa Usalama na Afya mahali pa kazi.

Akitoa taarifa ya maadhimisho ya mwaka huu katika siku ya kilele cha maadhimisho (Aprili 28, 2022), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za watu katika sehemu za kazi.

Aidha, alieleza kuwa kampeni ya mwaka huu imejikita zaidi katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na ushirikishwaji katika ngazi zote za maamuzi wakiwemo wafanyakazi ili nao wawe sehemu ya maamuzi na hivyo kujenga utamaduni wa kukinga zaidi kuliko kusubiri mambo yaharibike ndipo hatua za kuyarekebisha zichukuliwe.

“Utamaduni huu ukijengeka utapelekea kupunguza ajali, magojwa na vifo vinavyotokana na mazingira hatarishi ya kazi na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji ndani ya Taifa letu,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA, miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa katika kampeni ya uhamasishaji ya mwaka huu pamoja na; Mafunzo ya Usalama na Afya kwa wajasiriamali wadogo katika sekta mbali mbali wakiwemo wachimbaji wadogo, wazalishaji wa mazao ya misitu, wenye viwanda vidogo chini ya SIDO, watu wenye ulemavu pamoja na wanafunzi wa vyuo vya ufundi stadi na elimu ya juu.

Shughuli nyingine ni maonesho ya usalama na afya mahali pa kazi, shindano la tuzo za usalama na afya mahali pa kazi miongoni mwa maeneo mbali mbali ya kazi pamoja na ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya katika ofisi za Wizara na Ofisi mbali mbali za serikali.

Akihutubia mamia ya wakazi wa Dodoma na washiriki wa shughuli za maadhimisho kutoka katika mikoa mbali mbali nchini, Waziri Ndalichako ametoa wito kwa wadau wote wa masuala ya usalama na afya (Serikali, Waajiri na Wafanyakazi) kushirikiana katika kujenga utamaduni wa kuzuia vihatarishi vya usalama na afya kwa kuweka mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.

“Kwa ujumla ukiwauliza wafanyakazi sababu ya ajali kutokea, wengi wao watajibu ajali ni matokeo ya mazingira mabaya ya kazi na ukiwauliza waajiri wao watajibu kuwa ajali husababishwa na uzembe wa wafanyakazi. Hivyo, tunapoadhimisha siku hii leo, ni vema kuwahimiza wadau wote wawe na mjadala mpana wa namna ya kuimarisha utamaduni wa kuzuia vihatarishi miongoni mwa jamii yetu,” amesema Prof. Ndalichako.

Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani chimbuko lake ni iliyokuwa siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka waliopoteza maisha na kuumia kazini. Siku hiyo ya kuwakumbuka waathirika hao ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1996 huko Marekani katika jiji la Newyork.

Kwa hapa nchini, siku hii ambayo maadhimisho yake huratibiwa na serikali kupitia Taasisi ya OSHA yalianza kuadhimishwa mwaka 2004 ambapo kwa mwaka huu maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya 18.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post