POLISI DODOMA YATAKA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA UHALIFU WAKATI WA PASAKA

 Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA

 

KUELEKEA sikukuu ya Pasaka,Jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limewatahadharisha wananchi kuepuka tamaa ya ulevi wa kupindukia unaopelekea kufanya vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani.

 

Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi(SACP) Onesmo Lyanga amesema hayo leo jijini hapa na kueleza kuwa jeshi hilo limejipanga kuchukua tahadhari ya kutosha kukabiliana na wahalifu na kwamba halitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu watakaobainika kufanya vitendo viovu.

 

Mbali na hayo amepiga marufuku burudani kwa Watoto-Disko toto na kuwataka wazazi na walezi kuwaongoza Watoto wao wanapokwenda kwenye michezo au matembezi .

 

”Marufuku disko toto,Watoto wengi kulingana na umri wao wanashindwa kuhimili hali ya hatari inapotokea,kuna Watoto wengine ni watukutu wanaweza kutoroka hata nyumbani bila idhini ya wazazi,tuwaongoze vyema Watoto wetu ili kuwaepusha kwenye hatari,”amesema na kuongeza;

 

Nitumie nafasi hii pia kuwataka wamiliki wa kumbi zote za starehe kuepuka kujaza watu na kuhatarisha usalama,madereva wa vyombo vya moto mchukue tahadhari,zingatieni sheria za usalama barabarani,”amesema

 

Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa viongozi wa dini na kamati za ulinzi wa nyumba za ibada wasaidie kuimarisha usalama wa waumini kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

 

Katika hatua nyingine Jeshi la polisi mkoa wa Dodoma linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumiliki silaha mbili aina ya shortgun yenye namba 86387 na gobole lisilo na namba bila vibali,vipande vitano vya nondo vyenye muundo wa duara,ganda la risasi aina ya short gun na kopo la unga unaodhaniwa kuwa ni baruti.

 

Kwa mujibu wa SACP Lyanga, msako wa watu hao umefanyika mnamo 14/4/2022 katika Kijiji cha Ndogowe,Kata ya Ngambaku   wilayani Chamwino,mkoa wa Dodoma  na kuwataja  watu hao kuwa ni wenye umri wa miaka 35,45 na 60.


“Watuhumiwa hao ni wawindaji haramu wa nyara za serikali na tutawafikisha mahakamani mara upelelezi utakapokamilika,”amesema.

 

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post