SHEIKH MKOA WA MWANZA APINGA WATOTO KULELEWA KWENYE VITUOSheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke amepinga suala la watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakiwemo yatima kulelewa katika Vituo Maalum na badala yake watoto hao wakae na ndugu zao.

Sheikh Kabeke aliyasema hayo Jumamosi Aprili 16, 2022 wakati akizungumza kwenye kongamano la ‘malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa’ lililofanyika katika Msikiti wa Mkolani wilayani Nyamagana.


Pia Sheikh Kabeke ameongeza kuwa watoto wanaokimbilia mitaani hawapaswi kuchukuliwa na kupelekwa kwenye Vituo vya kulelea watoto bali wanapaswa kurejeshwa kwa wazazi, walezi ama ndugu zao kwani hayo ndiyo maadili tangu zamani.


“Kuwalea watoto kwenye vituo siyo afya, wanapaswa kulelewa na ndugu zao kama zamani ambapo mzazi alikuwa akifariki, mtoto anachukuliwa na baba mdogo, mama mdogo, shangazi au mjomba.” Alisema Sheikh Kabeke na kuongeza;


“Kwa sababu ya ubahiri, kila mtu siku hizi analea mototo wake, hana tabia ya kulea mtoto wa dada, kaka, babu. Na si lazima awe yatima, anaweza kuwa na wazazi lakini hawajimudu kiuchumi, unamchukua na kumsomesha na ndio maana BAKWATA tunasisitiza mtoto wa mwenzio ni wako” alisisitiza Sheikh Kabeke.


Aidha Sheikh Kabeke alijitolea mfano alivyolelewa na mjomba wake akisema hata jina ‘Kabeke’ analotumia ni la ujombani kwake ikiwa ni heshima ya malezi bora aliyopewa.


Katika hatua nyingine Sheikh Kabeke aliwataka wanandoa kurejea katika maadili ya dini, kuishi kwa upendo na kutotendeana ukatili wa kijinsia hatua itakayosaidia kuwalea vyema watoto na kuondoa changamoto ya watoto wanaokimbilia mitaani.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto KIVULINI, Yassin Ally alisema kutokana na maadili kuporomoka katika jamii, wazazi kutotimiza wajibu wa kufuatilia malezi na makuzi ya watoto, imesababisha watoto wengi kuingia katika vitendo hatarishi ikiwemo kukimbilia mitaani na kujihusisha na ulawiti ambapo alisema makongamano ya aina hiyo yatasaidia kuibadili jamii.


Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo akiwemo Abdul Kijonjoo na Bahati Mgosi walisisitiza wanajamii kurejea maagizo ya Mwenyezi Mungu yanayokataza kuwanyanyasa na kuwatelekeza watoto wakiwemo yatima na maskini na kwa kufanya hivyo itasaidia ndugu kukaa na watoto waliokimbilia mitaani ama walio vituoni.


“Wanaume wengi wana roho mbaya, unakuta wanaswali kila siku, wana sigma kubwa kama biskuti lakini matendo yao mabaya, waache tamaa ya kuzini watunze familia zao” alikemea Mgosi.


Kongamano hilo ni sehemu ya makongamano yaliyoratibiwa na BAKWATA Mkoa Mwanza kwa kushirikiana na shirika la KIVULINI kwa lengo la kujadili na kutafuta mbinu zitakazosaidia kurejesha maadili katika jamii, kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuondoa watoto wanaoishi mitaani ambapo yatafanyika katika Wilaya zote mkoani Mwanza.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke akizungumza kwenye kongamano hilo.

Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye kongamano hilo.

Mkurugenzi Mtendaji KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye kongamano hilo.

Waumini wa dini ya kiislamu katika Msikiti wa Mkolani (kulia) wakifuatilia mada kwenye kongamano hilo.

Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Abdul Kijonjoo akichangia mada kwenye kongamano hilo ambapo aliwaasa wanawake kuwa wabunifu katika ndoa zao ili kuwafanya waume zao wasishawishike kuwaacha na kukimbilia nje ya ndoa.

Mshiriki wa kongamano hilo, Sudi Shaban alisema kupata na kukosa kwenye ndoa ni jambo la kawaida hivyo wanawake wasipoachiwa matumizi mara moja moja wasilalamike bali wajiongeze kwa kutumia akiba inayokuwa imesalia siku ambazo mwanaume ameacha hela ya matumizi.

Naye Shamsa Ibrahim aliwasihi wanaume kuacha tamaa na kutulia na wake zao hatua itakayosaidia malezi bora katika familia.

Kwa upande wake Bahati Mgosi (kulia) aliwaasa wanaume kuzingatia misingi ya dini, badala ya kuswalimkila siku hadi kuwa na sigma kama biskuti huku wakiwa na roho mbaya kwani swala njema inaendama na matendo mema ikiwemo kuhudumia familia.

Mratibu wa zoezi la Anuani za Makazi Mkoa Mwanza, Abdul Mzee alitumia fursa ya kongamano hilo kutoa elimu kwa wananchi na kuwahimiza kutoa ushirikiano katika zoezi hilo kwani ni muhimu katika maendeleo ya taifa.

Waumini wa dini ya kiislamu wakifuatilia kongamano hilo ambapo waliaswa kuzingatia malezi bora kwa watoto wao ili kuondokana na watoto wanaokimbilia mitaani na kupunguza utoro mashuleni.

SOMA>>> Kongamano la BAKWATA Misungwi lafana

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post