NAIBU WAZIRI KATAMBI AIPONGEZA NSSF ILIVYORAHISISHA HUDUMA KWA WANACHAMA KUPITIA MIFUMO


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, ametembelea banda la NSSF akiwa na viongozi mbalimbali ambapo wameipongeza NSSF ilivyorahisisha huduma kupitia mifumo ya TEHAMA. Kutoka kushoto ni Lulu Mengele, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Anna Kitomari Afisa wa NSSF Dodoma na mwanachama wa NSSF ambaye pia ni mfanyakazi wa kampuni ya sigara, Abel Chinonga.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (watano kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NSSF. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro na Mwenyekiti wa Bodi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa NSSF. Kushoto ni Nuru Mbeyu ambaye ni Afisa TEHAMA wa NSSF.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Mfuko katika Maonesho ya OSHA kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga wakati alipotembelea banda la NSSF.
Tukio katika picha

Na MWANDISHI WETU

Serikali imepongeza kazi kubwa na mzuri inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika kuboresha huduma za wanachama kupitia mifumo ya TEHAMA ambazo zimekuwa rahisi na rafiki.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya Wiki ya Usalama Mahali pa Kazi yanayoendelea katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convetin Center jijini Dodoma.

Alisema NSSF imefanya maboresho makubwa kupitia mifumo ya TEHAMA inayomuwezesha mwanachama kupata taarifa mbalimbali za michango yake kiganjani kupitia simu ya mkononi bila ya kufika katika ofisi za NSSF.

“Ni mapinduzi makubwa sana ya kidigitali ambayo yamefanywa na NSSF katika utoaji wa huduma zake kwa wanachama, nawapongeza wafanyakazi wote kwa kazi mzuri wanayofanya.” Alisema.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Mstaafu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) Dkt. Adelhelm Meru, alipongeza maboresho makubwa yaliyofanywa na NSSF katika utoaji wa huduma kwa wanachama kupitia mifumo ya TEHAMA ambayo yanamrahisishia mwanachama kupata huduma kiganjani bila ya kufika ofisi za NSSF.

“Ninafurahi sana kufika katika hili banda la NSSF, nimejifunza mengi, nimefurahi kuona maendeleo mliyonayo lakini kilichonishangaza zaidi ni kuona kila kitu sasa mnakitoa kwenye makaratasi na kukiweka kiganjani,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Benard Kongwa, aliishukuru NSSF kwa namna inavyoongeza wigo wa kuwafikia wanachama, kutatua kero zao na kuboresha huduma za wanachama kupitia mifumo ya TEHAMA ambayo inaenda kuboresha upatikanaji wa huduma.

Mwanachama wa NSSF ambaye pia ni mfanyakazi wa kampuni ya Sigara, Abel Chinonga alisema huduma kiganjani ni rafiki na rahisi kwa kila mwanachama anayetumia kwani unaweza kupata taarifa mbalimbali zikiwemo za michango bila ya kufika ofisi za NSSF.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post