KAFULILA : VYOMBO VYA HABARI JIKITENI HABARI ZA UCHUNGUZI MUISAIDIE SERIKALI


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila (kushoto) akiongea na Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari mkoa wa Simiyu kwenye mdahalo wa Uhuru wa Kujieleza na Maadili ya Uandishi wa Habari, mdahalo huo umefanyika mjini Bariadi leo April 20, 2022.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi

VYOMBO vya Habari nchini vimetakiwa kuendelea kuandika habari za Uchunguzi ili viweze kuisaidia serikali kuwajibika na kufanya maamuzi yatakayosaidia kuchochoea Maendeleo na ustawi wa Taifa.


Aidha waandishi wa Habari pia wamesisitizwa kutumia vizuri taaluma zao ili waweze kuisaidia serikali pamoja na viongozi kuwajibika na kutimiza majukumu yao kwa manufaa ya jamii nzima.


Wito huo umetolewa leo na mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila wakati akifungua Mdahalo wa Wanahabari na wadau wa habari kuhusu uhuru wa kujieleza na maadili ya uandishi wa habari, uliofanyika katika ukumbi wa CK Mjini Bariadi.


Kafulila alisema waandishi wa habari waendelee kuandika na kufanya habari za uchunguzi ambazo zitaleta chachu ya uwajibikaji kwa mamlaka na taasisi mbalimbali.


"Msijione katika udogo bali mjione katika ukubwa, fanyeni habari za uchunguzi ili kuisaidia serikali kuongeza uwajibikaji…vyombo vya habari tusaidieni ili tujue tatizo lilipo, Rais anatamani ustawi na anachukia Rushwa’’,alisema Kafulila.


Aliongeza kuwa vyombo vya habari vikiwa mstari wa mbele vitaisaidia serikali kuchukua hatua na kwamba kwa sasa vimekuwa na mchango mkubwa sana katika kuchochea uwajibikaji ambao unasaidia kuleta Maendeleo kwa watanzania wote.


Aidha akiwasilisha mada kuhusu uhuru wa kujieleza, Mwezeshaji wa Mdahalo huo, Edwin Soko alisema uhuru wa kujieleza una manufaa makubwa kwa ustawi wa taifa, lakini lazima usivuke mipaka.

Soko aliwataka wadau wa habari kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi kwa weledi badala ya kunyimwa habari na kuwakosesha wananchi haki yao ya kupata habari.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu David Kafulila akizungumza kwenye mdahalo wa Uhuru wa Kujieleza na Maadili ya Uandishi wa Habari, uliofanyika ukumbi wa Ck mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari mkoa wa Simiyu Frank Kasamwa akizungumza kwenye mdahalo wa Uhuru wa Kujieleza na Maadili ya Uandishi wa Habari, mdahalo huo umefanyika mjini Bariadi leo April 20, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila (kushoto) akiongea na Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari mkoa wa Simiyu kwenye mdahalo wa Uhuru wa Kujieleza na Maadili ya Uandishi wa Habari, mdahalo huo umefanyika mjini Bariadi leo April 20, 2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments