MTOTO AUAWA KWA KUMWAGIWA MAJI YA MOTO AKIDAIWA KUJISAIDIA HOVYO NDANI YA NYUMBA YA BIBI YAKE


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtoto aitwaye Joseph Juma mwenye umri wa miaka minne mkazi wa kijiji cha Lyabukande kata ya Lyabukande wilaya ya Shinyanga ameuawa kwa kupigwa na fimbo kisha kumwagiwa maji ya moto ya kupikia ugali na bibi yake aitwaye Tatu Moshi kwa madai kuwa anajisaidia hovyo hovyo kwenye nyumba yake.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema tukio hilo limetokeaAprili 18,2022 majira ya saa 11 alfajiri katika kijiji cha Lyabukande kata ya Lyabukande wilaya ya Shinyanga.

“Mtoto aitwaye Joseph Juma mwenye umri wa miaka minne aliuawa kwa kupigwa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumwagiwa maji ya moto kabisa yaliyochemshwa kwa ajili ya ugali sehemu za tumboni na mguuni pia akiwa na mdogo wake aitwaye Limi Lameck mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 7 ambaye naye alipigwa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake bado na anaendelea kupata matibabu ya hayo majeraha”,amesema Kamanda Kyando.


“Aliyefanya tukio hili ni bibi yao aitwaye Tatu Moshi (45). Amekuwa akiwaadhibu wajukuu zake ambao mama yake ni Helena Nicholaus (21). Huyu Helena ni mtoto wa kwanza wa mama huyu na inasemekana amezaa na wanaume wawili alivyozaa akarudi nyumbani na kuishi na bibi huyo”,ameeleza Kamanda Kyando.


Amesema bibi huyo amekuwa akiwaadhibu vikali watoto hao kisa kwamba wanajisaidia hovyo kwenye eneo lake na kwenye nyumba yake.Majeraha tuliyomuona nayo marehemu mengine ni ya muda mrefu ‘makuukuu’ kwamba hicho kipigo hakikuanza jana bali ni cha siku nyingi.

Kamanda huyo amesema hata yule mtoto mdogo (Limi Lameck) naye ana majeraha ya muda mrefu, hii inaonesha kuwa bibi huyo alianza kutesa watoto hao muda mrefu.

“Huyu bibi tumemkamata na mama wa mtoto tumemkamata upelelezi ukikamilika tutawapeleka mahakamani”,amesema Kamanda Kyando.

"Hebu fikiria mtoto wa mwaka mmoja na miezi 7, mtoto wa miaka minne ambaye hajui jema wala baya unaadhibu kwa kipigo hiki, ni ukatili ulioje. Najua matendo haya yanafanyika sehemu mbalimbali hapa mkoani Shinyanga, natoa wito kwa wananchi kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake, sidhani kama haya mambo alikuwa anafanya kwa siri, majirani walikuwa wanajua hili jambo.

 Hebu angalia mama wa mtoto huyu alikuwa anaangalia tu watoto wake wanapigwa lakini hajatoa taarifa polisi wala kwa viongozi wa serikali ya kijiji. Hii ina maanisha wananchi wengi mnajua jirani anatesa watoto na hamtoi taarifa”,amesema Kamanda Kyando.

"Tupeni taarifa za matukio hata kwa siri, kama hutaki ujulikane nipigieni simu/sms au kunibipu 0739009957 mimi nitapiga, hii itatusaidia kupunguza ukatili dhidi ya watoto”,ameongeza Kyando.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments