MGONGOLWA : RAIS SAMIA AMEUPIGA MWINGI TUMUUNGE MKONO KWA NGUVU ZOTE

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Mjini mkoani Iringa, Joseph Mgongolwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza mwaka mmoja madarakani huku Watanzania wakitembea kifua mbele kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika sekta mbalimbali.

Mgongolwa ameyasema hayo leo Machi 20,2022 wakati akizungumzia mafanikio ya uongozi wa mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani na kutoa wito kwa wanachama na Watanzania wote kuendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameupiga mwingi sana,kila sekta ina jambo la kujivunia kutokana na uongozi wake mahiri, sisi makada na wanachama tunampongeza sana kwa kazi nzuri. Tunajisikia fahari kuona ndani ya mwaka mmoja wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani amefanya mambo mengi mno",amesema.

Pia amesema, kuna mambo mengi ya maendeleo,kiuchumi,kijamii na kisiasa yamefanyika ndani ya mwaka mmoja ambayo Watanzania wameyasikia na kuyaona ikiwemo miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

"Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameongeza usimamizi wa sera za soko huria, sera za kiuchumi na kifedha zenye mwelekeo wa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

"Ukitazama au kufanya tathimini ya haraka utagundua kuwa tangu Machi 2021 hadi leo Machi 2022, Tanzania imeongoza kwa kuvutia kiwango kikubwa zaidi cha uwekezaji kutoka nje kwa Ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kiwango cha uwekezaji kutoka nje kimeonekana kustawi kwa kasi. Hii ni hatua njema sana na inafaa kuungwa mkono kwa hali na mali ili kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kiuchumi,"amesema.

Pia amesema taifa la Tanzania lina bahati kubwa ya kumpata kiongozi mwanamke mwenye ujasiri, hodari na hofu ya Mungu katika kuwaongoza Watanzania na kuwatumikia.

"Mheshimiwa Rais Samia, ni kati ya wanawake ambao Mungu amewajalia karama ya kipekee katika uongozi, ni kiongozi ambaye ana uzoefu mkubwa, mwenye kuyajua mahitaji ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Rekodi hizi zinamuwezesha kupanga na kuelekeza nguvu katika mipango mbalimbali ya miradi ya maendeleo ili iweze kuwanufaisha Watanzania wote,"amesema Mgongolwa.

Amefafanua kuwa, mwaka mmoja wa Rais Samia akiwa Ikulu ameonyesha uwezo mkubwa na karama ya uongozi uliojaa ukomavu mkubwa wa kisiasa na maono makubwa,hekima na busara.

"Pia Mheshimiwa Rais Samia ana upendo na wananchi wake,ni kiongozi shupavu aliyeshiba dini na hofu ya Mungu, anachukia dhuluma na anataka kuona haki inasimama, hayo yote ni matunda mema ya kupata kiongozi mwenye uzoefu katika nafasi mbalimbali za utumishi.

"Chini ya uongozi wake imara na shupavu,kwa siku 365, Mheshimiwa Rais Samia amezidi kutufanya Watanzania wamoja bila kujali dini,ukabila, kanda, siasa na jinsia,"amesema Mgongolwa.

Amesema, Mheshimiwa Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kupitia serikali yake kuwajumuisha na kuyashirikisha makundi mbalimbali kutoka katika jamii ili yaweze kumsaidia kusimamia na kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo nchini.

"Kuanzia vijana, wazee,wanawake wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa, machifu, wafanyakazi na wakulima, wafanyabiashara na machinga, wanamichezo,wasanii na wengine wengi wamekuwa sehemu ya kumsaidia Mheshimiwa Rais Samia kufanikisha mipango mbalimbali ya kuleta maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema, mbali na kuimarisha uhusiano wa Kimataifa baina ya Tanzania na nchi za jirani, kikanda na jumuiya ya Kimataifa kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo diplomasia ya uchumi, Mheshimiwa Rais amefanikiwa kutafuta fedha ambazo zinatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya, maji, elimu, miundombinu na nyinginezo.

"Kwa msingi huo, nichukue nafasi hii kuwaomba makanda na wanachama wa CCM wakiwemo Watanzania wote kwa ujumla kujitokeza kila kona kuyaeleza mafanikio haya ili kutoa hamasa kwa jamii kushiriki zaidi katika shughuli za maendeleo. Ninaamini kupitia uongozi huu mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ifikapo Machi 2023, Taifa la Tanzania litakuwa na mafanikio makubwa mno,"amesema Mgongolwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments