DKT MABULA ATAKA KUTUNZWA MIUNDOMBINU STEDI MPYA YA MABASI ILEMELA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula Muonekano wa Stendi ya Mabasi na Maegesho ya Malori Nyamhongolo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza Muonekano wa majengo ya stendi ya Nyamhongolo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela


***********************


NA MUNIR SHEMWETA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wananchi wa Ilemela kuhakikisha wanaitunza miundombinu ya Stendi mpya ya mabasi na maegesho ya malori Nyamhongolo iliyo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela iliyokabidhiwa hivi karibuni kwa halmashauri hiyo jijini Mwanza.

Alisema, utunzaji miundombinu ya mradi huo wa stendi ya mabasi na maegesho ya magari utaiwezesha stendi hiyo kudumu kwa muda mrefu na kubainisha kuwa, uharibifu wowote utakaofanyika utakifanya kizazi kijacho kutokuwa na manufaa na stendi hiyo.

“Ukisikia historia ya mradi huu, Serikali ya Mhe Samia Suluhu Hassan imeweza kuwatendea haki wana Ilemela, tunamshukuru sana yeye pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela aliyepita John Wanga na timu yake sambamba na Mstahiki Meya Renatus Mulunga na Madiwani wa Halmashauri kwa kuhakikisha mradi umekamilika na kuanza kufanya kazi’’. Alisema Dkt Mabula.

Aidha, alimshukuru Mkuu wa wilaya ya Ilemela Hassan Masala na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa kupokea kijiti kutoka kwa watangulizi huku akikishukuru Chama cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela kwa kuisimamia vyema ilani ya chama iliyowezesha kutekelezwa mradi huo.

Kwa mujibu wa Waziri Dkt Mabula, mradi huo wa Stendi na Maegesho ya Malori unazo fursa mbalimbali zitakazowawezesha wananchi wa Ilemela na jamii kwa ujumla kufanya shughuli za kiuchumi kwa maendeleo yao, mkoa na taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii tarehe 11 Machi 2022 jijini Dodoma, Dkt Mabula alisema, kipindi ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani ameendelea kufadhili mradi huo uliogharimu takriban shilingi bilioni 26.3.

‘’Ninachoweza kuwaeleza wananchi wa Ilemela, mradi ule ni wa kimkakati na utanufaisha wana Ilemela, watu wa Mwanza lakini pia na jamii kwa ujumla kwa sababu mabasi yatakayokuwa yakiingia na kutoka ndani ya stendi yatakuwa yakitoka mikoa mbalimbali’’. Alisema Dkt Mabula

Alisema, stendi hiyo ya mabasi na maegesho ya malori ni ya aina yake na imesheheni huduma mbalimbali kama vile maeneo ya huduma za benki, maduka madogo ya bidhaa (mini super market) pamoja na migahawa itakayowawezesha wananchi kupata huduma pale wanapozihitaji.

‘’ Stendi imewekwa maduka takriban 74 ili kuwawezesha abiria wanaoshuka kununua vitu huku wenye mabasi wakitengewa ofisi kwa ajili ya kutoa huduma’’ alisema Dkt Mabula.

Akizungumzia fursa za wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga katika stendi hiyo, Waziri wa Ardhi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela alisema, halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inao mpango wa kujenga jengo kwa ajili ya wamachinga kufanya shughuli zao.

‘’Wamachinga nao watakuwa na jengo lao pembeni ya stendi maana mradi huu umekwisha na sasa tunategemea kuanza mradi mwingine wa machinga jirani na stendi’’ alisema Dkt Mabula.

“Tunajua eneo kama hili wamachinga wanahitaji kufanya biashara kwa kuwa ni stendi ya kisasa na mpango tulionao kama wana Ilemela tuna kiwanja kitakachojengwa machinga complex,” alisema Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post