JESHI LA POLISI LAFANYA UKAGUZI MABASI YA MIKOANI ILI KUPUNGUZA AJALI

Mkuu wa operesheni toka makao makuu kikosi cha usalama barabarani kamishana msaidizi wa polisi ACP Adam Maro akizungumza na madereva katika ukaguzi wa mabasi ya mikoani katika Stendi Kuu ya mabasi Arusha.

**
Na Rose Jackson,Arusha

Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani Makao Makuu ya Polisi kimeendesha Operesheni ya ukaguzi wa mabasi yanayobeba abiria katika stendi ya mabasi mkoa wa Arusha na kutoa elimu kwa madereva.

Akiongea na madereva wa mabasi yanayofanya safari zake toka mkoa wa Arusha kwenda mikoa mbalimbali ya Tanzania Mkuu wa Operesheni kutoka kikosi cha usalama barabarani Makao makuu Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Adam Maro ambaye ameongoza operesheni hiyo amesema wamefanya ukaguzi huo ili kupunguza ajali za barabarani.


Amewaasa kufanya ukaguzi wa vyombo vyao kabla ya kuanza safari ili kuepusha madhara ya ajali ambayo yanaweza kutokea kutokana na ubovu wa magari hayo.


Kwa upande wake Mkuu wa Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Solomon Mwangamilo amesema akiwa ni msimamizi wa sheria za usalama barabarani Mkoa wa Arusha hatakua na huruma wala kumuonea muhali dereva yeyote ambaye atafanya uzembe barabarani.


Naye Katibu wa Chama cha Kutetea abiria Kanda ya Kaskazini Godwin Mpinga amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara za madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

 George Joseph ambaye ni dereva ametoa wito kwa madereva wenzake kuhakikisha wanaendesha mabasi kwa kufuata sheria na kuacha tabia ya kusikiliza abiria wachahche wanaowashinikiza kutembea kwa mwendo kasi kwa lengo la kuwahi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments