AJIUA KWA KUJITUMBUKIZA KISIMANI BAADA YA KUUA MKE NA MTOTO MGOGORO WA MICHEPUKO

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Joseph Paul

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Madirisha Kanyalu (60) amejiua kwa kujitumbukiza kwenye kisima baada ya kumuua mtoto wake Meshack Madirisha (miezi 11) pamoja na mkewe aitwaye
 Evodia Nyerere (27) kwa kutumia kitu chenye makali akimtuhumu mkewe kuchepuka na wanaume wengine.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Joseph Paul tukio hilo limetokea Machi 2,2022 majira ya saa 12 asubuhi katika maeneo ya kitongoji cha Mwamadulu kijiji cha Bulambila kata ya Mwalukwa wilaya ya Shinyanga.

“Evodia Nyerere (27) na mtoto wake aitwaye Meshack Madirisha mwenye umri wa miezi 11 wakazi wa kitongoji cha cha Mwamadulu kijiji cha Bulambila kata ya Mwalukwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga waliuawa kwa kukatwa na kitu chenye makali sehemu ya shingoni na Madirisha Kanyalu (60) ambaye ni mme wa marehemu wakiwa ndani ya nyumba wanayoishi”,amesema Kaimu Kamanda Paul.

“Mtuhumiwa Madirisha Kanyalu alitoroka baada ya tukio na kwenda kujitumbukiza kwenye kisima cha maji kilichopo karibu na nyumba yake aliyokuwa anaishi na kufariki dunia”,ameeleza.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia ambapo Madirisha Kanyalu alikuwa anamtuhumu mke wake kuwa na mahusiano ya wanaume wengine.

“Natoa wito kwa wanandoa/wenza wapeleke malalamiko yao mapema kwenye madawati ya jinsia na watoto yaliyopo vituo vya polisi pamoja ustawi wa jamii ili kupata suluhisho la migogoro yao”,amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post